Hili la Kongani za Viwanda Kila Wilaya, Dkt.Samia umepiga Penyewe

GEORGE MARATO TV
0


Na: Dkt. Reubeni Lumbagala, Tanga

Viwanda ni moja ya sekta za kiuchumi zenye mchango mkubwa katika kuchechemua maendeleo ya watu na ya Taifa. Uwekezaji wa viwanda unakwenda sambamba na uboreshaji wa sekta nyingine kama vile kilimo, umeme, maji, barabara, biashara ili kwa pamoja viwezeshe ufanisi wa viwanda.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeipa msukumo mkubwa sekta ya viwanda. Ndiyo maana kumefanyika maboresho makubwa ya sheria zinazosimamia uwekezaji na biashara, uboreshaji wa mazingira ya kufanyia shughuli za viwanda na biashara pamoja na uwekaji wa kodi rafiki ili kuvutia shughuli za viwanda na ustawi wake.

Moja ya ahadi iliyomo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2025-2030 ni uanzishwaji wa kongani za viwanda (industrial parks) kila wilaya hapa nchini ili kuchochea huduma za kijamii, maendeleo ya kiuchumi na Taifa kwa ujumla. Kongani za viwanda ni maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za viwanda. Katika maeneo hayo huwepo viwanda vya mfano na huduma zote muhimu za kuwezesha ufanisi wa uzalishaji viwandani.

Kutokana na umuhimu wa kukuza uchumi wa wananchi na Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM amedhamiria kuhakikisha azma ya kuwa na kongani za viwanda kila wilaya katika kipindi cha miaka mitano ijayo 2025-2030 inafanikiwa kikamilifu.

Septemba 4, 2025, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Mbeya Mjini katika kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mambo mengine, aliahidi kujenga kongani za viwanda ili kusaidia kukuza kilimo, ajira, biashara na uchumi kwa ujumla. "Tunakwenda kuweka kongani za viwanda ili vijana wa Mbeya waongeze thamani mazao yao na tunakwenda kuyauza sokoni wapate faida zaidi," amesema Dkt. Samia.

Uwepo wa kongani za viwanda kila wilaya unakwenda kuleta mapinduzi makubwa ya uchumi kwani wakulima wa mazao mbalimbali watapata uhakika kuuza mazao yao. Vilevile, wafugaji watapata masoko ya mazao ya mifugo yao kwani uanzishwaji wa kongani za viwanda utazingatia upatikanaji wa malighafi katika wilaya husika. Vijana watapata fursa za ajira katika viwanda hivyo, jambo litakalosaidia kupungua kwa tatizo la ajira nchini. Vilevile, biashara mpya zitafunguliwa kama migahawa kwa ajili ya kuwauzia vyakula wafanyakazi viwandani.

Septemba 13, 2025, Mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, nae ameeleza azma ya CCM kuhakikisha kila wilaya inakuwa na kongani ya viwanda. "Tumesema tunaenda kutengeneza kongani za viwanda nchi nzima kwenye wilaya zote kwa kuzingatia kila wilaya inazalisha nini. Kama ninyi ni wafugaji wakubwa sana tunaenda kuweka kiwanda cha kusindika nyama, kama ni wakulima tunaweka kiwanda cha kutengeneza vyakula vya mifugo," amesisitiza Dkt. Nchimbi.

Kuelekea Oktoba 29, 2025, ambapo Uchaguzi Mkuu utafanyika, kuna kila sababu ya wananchi kuchagua wagombea watokanao na CCM kuanzia nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani ili kwa pamoja waweze kushirikiana kikamilifu kufanikisha mikakati kabambe wa uanzishwaji wa kongani za viwanda kila wilaya ili kuchochea zaidi maendeleo ya wananchi na kukuza pato la Taifa.

Maoni: 0620 800 462.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top