Mradi wa Tactic Manispaa ya Kibaha Kuongeza Fursa za Uchumi Kwa Wananchi

GEORGE MARATO TV
0


Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA ) inatarajia kuleta manufaa makubwa kwa Manispaa ya Kibaha Mkoani Pwani na Miji mingine nchini, kupitia Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) ukitajwa kuongeza fursa za ajira kwa Vijana na kuchochea uchumi wa Manispaa ya Kibaha chini ya Maboresho makubwa ya mazingira ya ufanyaji wa biashara yatakayofanyika.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Septemba 25, 2025 katika Soko la Mnarani, Kibaha na Mhandisi Emmanuel Manyanga, Muwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARURA ambaye pia ni mratibu msaidizi wa mradi wa TACTIC wakati wa utiaji saini Mkataba wa mradi wa TACTIC kwa Manispaa ya Kibaha ukihusisha Uboreshaji wa Miundombinu ya Barabara, Soko kuu la Mnarani, Bustani ya Mapumziko na burudani pamoja na ujenzi wa Jengo la Usimamizi wa mradi ukigharimu shilingi Bilioni 19.83 bila jumuisho la kodi ya ongezeko la thamani (VAT)

"Mradi huu kwa Manispaa ya Kibaha utaongeza fursa za ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi, kuboresha hali za biashara katika maeneo husika na hivyo kuchangia maendeleo ya muda mrefu ya jamii na Taifa kwa ujumla. Pia huduma za usafiri na usafirishaji zitarahisishwa pamoja na  kupendezesha Manispaa hiyo inayokua kwa kasi na kuipa hadhi inayostahili," amesema Mhandisi  Manyanga.

Aidha alieleza kuwa Mradi wa Uendelezaji Mji wa Kibaha kwa awamu ya kwanza uliosainiwa leo unatekelezwa na Mkandarasi M/s Dimetoclasa Real Hope Limited kwa gharama ya shilingi 19, 832, 922, 855.99, ukitarajiwa kutekelezwa kwa miezi 15 na unahusisha ujenzi wa barabara za Tughe-Anglikana (Km 1.1), Barabara ya picha ya ndege- Hospitali ya Lulanzi (Km 3.7) pamoja na ujenzi wa Soko la Mnarani. Pia mradi utajenga bustani ya kisasa pamoja na jengo la usimamizi na uratibu wa Mradi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge ametoa Wito kwa Wananchi wa Kibaha Mkoani Pwani kuitunza miundombinu inayotekelezwa na Mradi wa TACTICS akielekeza Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kufanya tathmini ya miradi yenye kujiendesha yenyewe ikiwemo Masoko na Vituo vya Mabasi ili kuhakikisha miradi hiyo inatumika kuboresha huduma na kuongeza mapato ya Halmashauri na Serikali.

"Ni matarajio yetu sote kuwa miradi hii italeta mabadiliko chanya kwa Wananchi wa Manispaa yetu ya Kibaha na wageni ambao watafaidi huduma za mahitaji mbalimbali ya usafiri na usafirishaji, manunuzi ya vyakula, mavazi pamoja na mazingira bora ya kibiashara kwani ni dhahiri kuwa thamani ya maeneo husika itapanda na hivyo kusababisha ongezeko la mapato kwa Halmashauri yetu,” alisema Kunenge.

Aidha Mhe. Kunenge ametoa rai kwa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa haraka, ubora uliokusudiwa na kukamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba na mpango kazi uliokubalika ili wananchi waanze kunufaika na miundombinu hiyo ambayo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza katika Manispaa ya Kibaha.

Mradi wa TACTIC ni mojawapo ya miradi inayofadhiliwa na serikali kuu kupitia Mkopo wa Benki ya dunia wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 410 bila VAT, malengo ya mradi huu yakiwa kuboresha miundombinu ya Miji 45 ya Tanzania pamoja na kujengea uwezo   Halmashauri ili ziweze kujiimarisha katika usimamizi wa uendelezaji Miji pamoja na ukusanyaji wa mapato.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top