Na MASHAKA MHANDO, Tanga
KIKUNDI cha akinamama wa dhehebu la bohora Isinasher ya Jijini Tanga, kimemkabidhi mashine mbili za cherahani dada Halima Mohamed mwenye ulemavu wa viungo.
Wakikabidhi mashine hizo zenye thamani ya sh. 1, 400,000, mmoja wa akina mama hao Fatema Mamujee alisema kikundi chao kilijipanga kukabidhi mashine hizo kwa kikundi au mtu mwenye mahitaji yanayohitaji msaada.
Mamujee alisema wanamshukuru Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batlida Salha Burian kwa kumuibua dada Halima ambaye kiukweli alihitaji msaada huo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo, Halima ambaye anatumia kiti mwendo kufanya shughuli zake za kiuchumi, alisema kazi ya cherahani ameianza toka akiwa na miaka 14.
Alisema ndoto yake ilikuwa ni kumiliki mashine ya kushoenea nguo yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha kiwango anachokihitaji kwajili ya kukidhi mahitaji ya maisha yake lakini pia na familia yao.
alisema msaada huo umekuja wakati muafaka na kwamba hata kiwango cha nguo alichokuwa akishona kitaongezeka mara dufu na hivyo kuwashukuru kwa namna ambavyo waliona yeye ni mtu mwenye uhitaji.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Salha Burian naye ameahidi kukabidhi mashine nyingine mbili kwa lengo la kuiinua jamii hiyo lakini pia atahakikisha kunapatikana jengo maalum ili kuwakusanya Wanawake hao wenye mahitaji maalum ili wafanye shughuli zao katika eneo moja.
"Kuna majengo yapo maeneo jirani tutaangalia namna ya kupata mojawapo ili kuwakusanya ndugu zetu hawa, wataendeshea shughuli zao hapo huku tukiwasaidia kupata wateja" alisema Mkuu wa Mkoa wa Tanga.



.jpg)
.jpg)






