Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mwanasiasa Mkongwe nchini, Stephen Masatu Wasira amechaguliwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho tawala - upande wa Tanzania Bara.
Mkutano huo umefanyika leo Januari 18, 2025 jijini Dodoma, ukiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt Samia Suluhu Hassam, ambapo Wasira amepigiwa kura za ndiyo 1,910 sawa na asilimia 99.42 ya kura halali 1,917 huku kura 7 zikimkataa.
Jina la Wasira lilipendekezwa na kikao cha Kamati Kuu ya CCM Taifa jana, kisha kuwasilishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambayo nayo kupitia kwa Mwenyekiti Rais Samia imeliwasilisha kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa leo kwa ajili ya kupigiwa kura za ndio, au hapana.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Wasira amewashukuru wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa chini ya Mwenyekiti Rais Samia, kwa kumuamini na kumpa heshima ya kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.
Wasira ameahidi kuanza kutumikia wadhifa huo kwa kutekeleza falsafa ya R nne (4R) ya Rais Samia inayojikita katika masuala ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms) na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).
Wasira amechukua nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara baada ya Abdulrahman Kinana aliyekuwa anaishikilia kuomba kupumzika mwaka Jana.
Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa umeahirishwa hadi kesho Januari 19, 2025 utakapoendelea na ajenda zilizobaki.