Na Shomari Binda-Musoma
WAZIRi wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti, Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawe amesema ameshuhudia mambo makubwa ya maendeleo kwenye jimbo la Musoma vijijini na mjini.
Kauli hiyo ameitoa leo oktoba mosi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mara sekondari mara baada ya kufanya ziara kwenye majimbo hayo.
Amesema serikali imekuwa ikileta fedha nyingi mkoani Mara na zimetumika vizuri na kuwaletea wananchi maendeleo.
Waziri huyo amesema vijana wanayo nafasi ya kufahamu shughuli za maendeleo inayotekelezwa na wasidanganywe na watu wanaopotosha.
" Waheshimiwa wabunge wote wawili Profesa Sospeter Muhongo wa jimbo la Musoma Vijijini na mheshimiwa Vedastus Mathayo hapa mjini niwashukuru kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kusukuma shughuli za maendeleo.
" Changamoto nilizosikia ntazifikisha moja kwa moja kwa mheshimiwa Rais na naamini zitafanyiwa kazi",amesema
Amesema kikubwa ni kuendelea kumuombea Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwaletea wananchi maendeleo mkoani Mara.
Mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo amesema yapo mambo mengi ya kimaendeleo yamefanyika jimboni humo na kinachotakiwa ni wananchi kuwezeshwa kiuchumi.
Amesema Musoma kulikuwa na viwanda vingi vikiwemo vya nguo,samaki,maziwa lakini kwa sasa vimekufa na kuomba serikali kuona namna ya kuvifufua.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo amemuomba Waziri George Simbachawene kufikisha salam kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyopeleka fedha nyingi kwa wananchi wa jimbo hilo kwaajili ya miradi ya maendeleo.
Amesema serikali imefafanya uwekezaji mkubwa kwenye hospitali kuu ya jimbo hilo iliyoko kwenye Kitongoji cha Kwikonero Kijijini Suguti aliyoitembelea na kuweka jiwe la msingi
Muhongo amesema gharama za uwekezaji hadi leo kwa ujenzi ni shilingi bilioni 3.53,vifaa tiba zaidi ya shilingi bilioni 2.00 ikiwekwa X-ray, ultrasound, oxygen plant na vingine
Waziri huyo yupo mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya siku 4 kwaajili ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.