Uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili umefanya ziara ya kikazi nchini Comoro kwa mwaliko wa Jeshi la Comoro, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuanzisha ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya afya, hususan huduma za hospitali ya jeshi.
Ziara hiyo iliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt. Delilah Charles Kimambo, na ilihusisha mikutano ya kitaalamu na Hospitali ya Jeshi la Comoro pamoja na viongozi waandamizi wa jeshi hilo. Katika ziara hiyo, ujumbe wa Muhimbili ulipata fursa ya kutembelea miundombinu ya hospitali, kukagua vifaa tiba vilivyopo, na kujadiliana kwa kina kuhusu hali ya utoaji wa huduma za afya na maeneo yanayohitaji kuboreshwa.
Jeshi la Comoro limeialika Hospitali ya Muhimbili kwa lengo la kuanzisha ushirikiano utakaohusisha menejimenti ya hospitali, huduma za kibingwa na kibingwa bobezi, uboreshaji wa vifaa tiba, tiba shirikishi, pamoja na maeneo mengine muhimu yatakayochangia kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za afya kwa wanajeshi na raia wa Comoro.
Ziara hiyo iliratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro, ambapo Balozi Saidi Yakubu aliungana na ujumbe wa Muhimbili katika shughuli zote za ziara, akisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania kuendeleza diplomasia ya afya na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, uongozi wa Muhimbili ulieleza utayari wa hospitali hiyo kushirikiana na Hospitali ya Jeshi la Comoro katika kuboresha mifumo ya uendeshaji wa hospitali, kuimarisha rasilimali watu kupitia mafunzo na uhamisho wa ujuzi, pamoja na kusaidia katika uanzishaji wa huduma za kibingwa ambazo kwa sasa hazipatikani nchini humo.
Ziara hiyo inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Comoro katika sekta ya afya, sambamba na kuimarisha uhusiano wa kindugu na kimkakati kati ya mataifa hayo mawili.






