Usilolijua Kuhusu Jenista Mhagama!

GEORGE MARATO TV
0


 *Ameandika Askofu Mwamakula* 🙏🙏🙏

Usilolijua Kuhusu Jenista Mhagama!

Nusu ya pili ya mwaka 2023 ilikuwa na joto la aina yake katika siasa za Tanzania. Fenomena ijulikanayo kama Boniface Anyisile Mwabukusi ilianza kuchomoza na kung'ara katika siasa za Tanzania kupitia sakata la Mkataba wa Bandari.

Mwabukusi, Dkt. Slaa na Mdude waliwekwa kizuizini kule Mbeya baada ya IGP kutangaza kuwa kuna watu walitaka kuipindua serikali ya Rais Samia. Askofu Mwamakula alijikuta akiwa katikati ya utetezi wa watu hao. Walitamkiwa makosa ya uhaini, lakini ghafla wakaachiwa wakiwa polisi bila ya kufikishwa mahakamani.

Alphonce Lusako Mwamwile na mawakili wenzake walifungua kesi ya kupinga mkataba huo. Mwabukusi na wenzake wakawa mawakili wao. Lakini kesi ilitupwa mahakamani kwa kile kilichoelezwa na jaji kuwa mahakama haikuwa na mamlaka ya kuingilia mamlaka ya Bunge.

Mwabukusi na wenzake kadhaa wakahamishia mapambano nje kwa kutangaza maandamano. Mwabukusi alianza kusakwa kama 'dhahabu ya Chunya' na wenye mamlaka. Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida, Kikosi cha askari kama 15 walifika usiku wa manane katika makazi ya Askofu Mwamakula kule Itunge, Kyela wakidai kumsaka askofu kwa madai kuwa alikuwa kule kwa ajili ya kuandaa maandamano! Chubhaa!

Siku mbili baadaye, Jenista alituma ujumbe na kumualika Askofu Mwamakula bungeni. Ilibidi ndugu wa askofu wajadili kwa kina kumshauri kama aende au la. Lakini cha kushangaza sana Jenista alisema hawakujua kabisa kama kuna watu walikuwa wanamfuatilia askofu nyumbani  alipiga simu kwa RPC wa Mbeya kujiridhisha ili kama ni kweli: tuyaache hayo ni 'syapatali'! Na hatimaye Askofu Mwamakula alitinga Bungeni, alitambulishwa na Spika Dkt. Tulia Ackson ya kuwa ni mgeni wa Waziri Mkuu! 

Baadaye askofu na wenzake watatu: Rev. Dr. Fr. Charles Kitima (TEC) na Askofu Dkt. Kalikawe Lwakalinda Bagonza walikutana pia na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu katika kikao cha faragha. Waziri Mkuu aliyepatia salaam za Rais Samia. Kikao kile kilipoisha, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama alimuombwa Askofu Mwamakula ili abaki kwa ratiba ya kikao kingine pamoja naye kesho yake.

Kikao cha waziri na askofu kilikuwa na agenda mbili: mambo ya Kanisa na suala moja nyeti. Suala hilo nyeti lilimhusu Boniface Mwabukusi. Inaonekana serikali ilijua kuwa askofu alikuwa karibu na Mwabukusi. Askofu alitumia nafasi ile kwa ajili ya kushauri serikali isimuwinde  Mwabukusi kwa kuwa hakuwa na madhara kwa taifa. Alisisitiza kuwa wamuache awe anasema kwa kuwa ni haki yake lakini pia kama atazuiwa atakuwa na madhara zaidi. Kama watu katika jamii wataminywa bila kusema, jamii italipuka! Jenista alielewa na kuahidi kufanyia kazi kwa kuwashauri wenzake.

Jenista alisikiliza kwa makini lakini alitoa ombi moja kuwa askofu amueleze Mwabukusi aache kushambulia watu binafsi katika hoja zake. Lile halikuwa jambo gumu kwa askofu. Serikali kwa kiasi kikubwa iliacha au ilipunguza kumuwinda Mwabukusi na yeye alijikita katika kujenga hoja zake kwa staha zaidi bila kupunguza ukweli.

Kwa ujumla, kikao kile kilikuwa na umuhimu wa kipekee. Mazungumzo yetu na Jenista yalileta suluhisho fulani. Serikali iliweza kwa mara ya kwanza kuelewa jambo lililoifanya upunguze au iache kumfuatilia Mwabukusi kwani kwa kumtafuta kulileta taharuki kubwa na kuifanya serikali izidi kuchukiwa zaidi na wananchi.

Leo nimesikia taarifa za kifo chake. Kama njia ya kuenzi mambo muhimu tuliyowahi kujadili naye nimeamua kutoa ushuhuda huu. Na kama Mungu atanipa kibari nitaeleza mengine jinsi Jenista alivyoshiriki kutuliza mambo ambayo kama yangeangukia mikononi mwa baadhi ya 'vichaa wa mfumo' hali ingekuwa mbaya sana.

Katika mambo magumu sana, Jenista alitafuta ushauri na aghalabu alinitafuta. Wenzie wengi hawakumuelewa kwa kuwa karibu na mimi kwa kuwa walilishwa matango kutoka kule Madaba kuhusu mimi. Lakini wapo walionitahadharisha mimi pia kuhusu 'Mama wa Peramiho'! Sikuwa na la kuogopa kwa kuwa ukiwa mtetezi wa haki unatumia njia yoyote ya haki na ya heshima ili kuwasaidia unaowatetea lakini pia kuwafanya watesi wawaelewe watu wengine ambao wao wanawakandamiza. Nilitimiza wajibu wangu na ndio maana sikuwahi kuogopa kukutana naye.

Jenista alikuwa kama daraja muhimu sana na pia kwa sababu ya unyenyekevu aliokuwa nao. Kama mtu wa mfumo hawezi kukwepa mapera ya mfumo, lakini alikuwa na umuhimu wake. Ni muhimu watu wakajua kuwa panapokuwa na uhasama na makundi katika jamii ni lazima pia wapatikane watu wa kuvunja uhasama huo na hata kuyaunganisha makundi - hili ni jukumu la hatari sana na lililo gumu. Nilijitahidi kulifanya kwa gharama kubwa ikiwemo kutokueleweka!

Ninakulilia Jenista, umeondoka kabla ya kuona kile ambacho nilitamani ukione - Tanzania ile ambayo mtu atapata madaraka ya uongozi kwa njia ya haki, heshima ya kura itakaporudishwa. Uliniita dada, nilikuita kaka! Yule 'mdogo' wako amejawa na majonzi sana. Inaonekana wewe haukumuaga. Na yule 'kaka' yako ambaye ni Mchungaji wa Milima ya Uchagani ameshikwa na mshangao. Mungu akayakumbuke mema yako! Ulale salama Jenista! Nimejitahidi kwa upande wangu kuandika kile ambacho hakuna wa kukisema kuhusu wewe. Hata ningefika msibani kwako huko Dodoma au Peramiho, nisingeweza hata kupewa 'maiki' ili 'niropoke' maana unajua jinsi 'Wangindo' wanavyoogopa 'waropokaji' kama mimi. 


Nitaropoka mengine kwa faida ya 'Wapangwa' na 'Wanyasa'! Lakini wapo pia uliowasaidia ila hawakujua kwa kuwa uliwapambania kwa siri. Ndio dunia ilivyo dada! Tutaonana 'Madaba'!

Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!

Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula 

Itunge, Dar es Salaam; 11 Desemba 2025; Saa 9:26 alasiri

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top