Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Mlimba (CCM), Dk Kellen-Rose Rwakatare amewahimiza wazazi kushirikiana na walimu katika malezi ya watoto wao badala ya kuona jukumu hilo kama ni la walimu.
Alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa tamasha la kitaaluma na michezo kwa wanafunzi wa shule ya St Mary’s Tabata .
Dk Rwakatare ambaye pia ni Mkurugenzi wa shule za St Mary’s alisema kama wazazi wanatona umuhimu wa kuzingatia malezi bora kwa watoto wao, basi kwa kushirikiana na walimu watapata taifa lenye nidhamu kubwa.
“Tusione kuwa tunapolipa ada tunakuwa tumemaliza, mwalimu anasehemu yake ya malezi lakini mzazi anasehemu kubwa kwasababu muda mwingi anakuwa na mtoto nyumbani,” alisema
Kwenye tamasha hilo, wanafunzi walionyesha umahiri wa vipaji mbalimbali kuanzia vipaji vya taaluma na vipaji vya michezo ya aina mbalimbali ambapo baadhi ya wanafunzi hao walimudu kuimba nyimbo mbalimbali kwa lugha ya kichina.
Dk Rwakatare alisema kila mwaka wamekuwa wakiandaa matamasha kama hayo na mwaka huu shule hiyo inatimiza miaka 8 tangu kuanzishwa kwake.
Alisema wameamua kuwa na tamasha hilo ili kuonyesha vipaji mbalimbali ambavyo watoto wa shule hiyo wanavyo kuanzia vipaji vya kitaaluma, kuimba na kucheza nyimbo za makabila mbalimbali.
“Watoto wa St Marys wanafundishwa mambo mbalimbali kuanzia sayansi na teknolojia na wameonyesha vipaji vya aina mbalimbali kama ambavyo mmeshuhudia wenyewe kwenye maonesho ya leo,” alisema Dk Rwakatare
Alisema shule za St Mary’s zimejikita kufundisha kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia duniani kwa kufundisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA ili kuendana na kasi ya ulimwengu kuhusu teknolojia.
Aidha, alisema shule hizo zimekuwa zikifanya vizuri kitaaluma kwa muda mrefu na kwa mwaka huu wanafunzi wake wote waliofanya mtihani wa darasa la saba wamefaulu kwa wastani wa alama A.
“Kwenye shule zetu zote wanafunzi wamepata wastani wa A sasa hii inaonesha ni kwa kiasi gani shule zetu ziko juu kitaaluma kwa hiyo tunaomba wazazi waendelee kutuamini kwa kutuletea watoto wetu wasome shule za St Mary’s,” alisema
Alisema shule hiyo imekuwa ikifundisha ujuzi wa aina mbalimbali kuendana na mitaala mipya ili wanafunzi wanapomaliza shule wawe na ujuzi wa kujiajiri kwenye fani mbalimbali badala ya kuhangaika kutafuta ajira.






