MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira amewahakikishia wananchi wa Pangani kwamba miaka mitano ijayo katika utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi ya 2025-2030 itabeba neema kubwa kwa maendeleo ya wilaya hiyo.
Miongoni mwa neema hizo ni pamoja na kukamilika kwa barabara ya Tanga-Pangani-Bagamoyo kupitia Saadani ambayo itafungua uchumi wa wilaya hiyo na mkoa wa Tanga kwa ujumla.
Wasira aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wana CCM waliojitokeza kwa wingi katika mkutano wa ndani wa Chama uliowashirikisha viongozi wa wilaya hiyo na mkoa wa Tanga kwa ujumla.
Alisema mbali na barabara, pia miaka mitano ijayo iwapo CCM itachaguliwa kurudi madarakani serikali yake itaongeza shule za msingi, sekondari, zahanati na vituo vya afya.
Aidha, Wasira amewapokea wanachama wapya 153 waliohamia CCM kutoka vyama mbalimbali vya siasa akiwemo Katibu wa ACT Wazalendo...
Awali, Wasira amesema kazi kubwa iliyopo mbele ya wana CCM ni kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura na kuwashawishi wasiokuwa wanachama kufanya hivyo kuihakikisha dunia kwamba Tanzania ipo tayari kwa uchaguzi mkuu.
Akizungumza na wana CCM waliojitokeza kumpokea Uwanja Ndege wa Tanga, Wasira mesema dunia inaitupia jicho Tanzania kuona kama Watanzania wapo tayari kwa uchaguzi na kigezo kikubwa ni mwitikio wao Oktoba 29, mwaka huu kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura kuchagua viongozi wao hususan mgombea urais kwa tiketi ya CCM Dk. Samia Suluhu Hassan, wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na Chama.
"Kwa hiyo kazi yangu ya kwanza nawaomba wana CCM na wapenzi wa Chama chetu katika mkoa wa Tanga. Ikifika tarehe 29 (Oktoba 2025) mjitokeze kwa wingi sana kwenda kwenye vituo vya kupigia kura kwa sababu dunia inataka kujua je watu wanapiga kura au hawapigi, mimi nina imani na watu wa Tanga mtatoka kwenda kupiga kura," alisema.
Wasira ametumia ziara hiyo kumwombea kura Dk. Samia, Mgombea ubunge wa Jimbo la Pangani Jumaa Aweso, wagombea ubunge wengine wa jimbo hilo, pamoja na wagombea udiwani waliosimamishwa na Chama.