Wasira Awanyooshea Kidole Wanaojipanga Kwa Umeya, Uenyekiti wa Halmashauri Badala Kusaka Ushindi wa Ccm

GEORGE MARATO TV
0


Na Mwandishi Wetu, Mkinga

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amewaonya baadhi ya wagombea udiwani katika maeneo mbalimbali ambao wameanza harakati za kusaka uenyekiti wa halmashauri na umeya, kabla ya uchaguzi.

Amesema wanachotakiwa kufanya wana CCM wote kwa sasa ni kuhakikisha wanasaka kura za kishindo kwa Chama hususan za mgombea urais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amesema hayo leo Septemba 25, 2025 alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM katika kikao cha ndani kilichofanyika wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga, jana.

Kikao hicho ni mfululizo wa vikao anavyoviendesha kwa kukutana na viongozi na wana CCM kumwombea kura Dk. Samia, wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na Chama kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

"Kwa madiwani ninawaomba sana sio hapa Mkinga, hapa sijaambiwa lakini huko nilikotoka madiwani wameanza kutafuta mwenyekiti wa halmashauri na huku wao wenyewe hawajachaguliwa, sasa wewe utajuaje kama utachaguliwa wewe uanze kutafuta mwenyekiti wa halmashauri.

"Acheni mambo ya kutafuta mwenyekiti wa halmashauri kwanza tuchaguane halafu mambo ya mwenyekiti wa halmashauri yatakuja baadaye," ameagiza.

Amesema hata nafasi ya umeya hutazamwa kupitia vikao vya juu na kwamba katika mchakato wake iwapo atabainika diwani alianza mapema Chama hakitasita kumwengua katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi hiyo.

"Wameanza, ninawaambia hapana, hata umeya tunatazama kwenye kamati, nitasema nilikwenda Mkinga (ni mfano) nikawaambia lakini hawakunisikiliza na huyu ndiye alikuwa anaongoza kampeni, tunamfuta tunaweka yule ambaye alikuwa ametulia.

"Siwatishi nawaambia maneno ya kweli na maneno ya kweli nayo yana ncha kali yanaweza kuonekana kama kitisho," amesisitiza.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top