Riek Machar Ashtakiwa kwa Uhaini Sudan Kusini

GEORGE MARATO TV
0

Juba, Sudan Kusini 

Hali ya kisiasa nchini Sudan Kusini imeingia katika mtafaruku mpya baada ya serikali kutangaza rasmi mashtaka ya uhaini dhidi ya Makamu wa Kwanza wa Rais aliyesimamishwa, Riek Machar Teny.

Mashtaka hayo mazito yanajumuisha uhaini, mauaji, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, kutokana na mashambulizi ya Machi mwaka huu katika mji wa Nasir, Jimbo la Upper Nile na kusababisha vifo vya said ya wanajeshi Mia mbili.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu, mashambulizi hayo yalitekelezwa na wanamgambo wa White Army ambapo watu kadhaa waliuawa na mamia kujeruhiwa. 

Serikali ya Rais Salva Kiir Mayadit inadai kuwa mashambulizi hayo yalikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Machar, ambaye kwa muda mrefu ameonekana kama kiongozi wa kisiasa mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa wapiganaji hao.

“Ushahidi wetu unaonyesha wazi kwamba Dkt. Machar alihusika katika kuratibu na kusapoti mashambulizi hayo. Serikali haiwezi kukaa kimya mbele ya vitendo vya kuvuruga amani na kuhatarisha maisha ya wananchi,” alisema msemaji wa serikali katika taarifa iliyosomwa kwa vyombo vya habari mjini Juba.

Tangu mwezi Machi, Machar amekuwa chini ya kizuizi cha nyumbani, na wiki iliyopita Rais Salva Kiir Mayardit alimsimamisha rasmi kutoka wadhifa wake kama Makamu wa Kwanza wa Rais. Hatua hiyo imesababisha mtikisiko mkubwa ndani ya serikali ya umoja wa kitaifa, ambayo ilibuniwa kupitia makubaliano ya amani ya 2018 yaliyolenga kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyochukua zaidi ya miaka mitano.

Upande wa Machar, hata hivyo, umejitokeza kupinga vikali mashtaka hayo, ukidai kuwa ni ya kisiasa na yanalenga kumdhoofisha kisiasa. 

“Hii ni njama ya wazi ya kumweka kando kiongozi ambaye amesimama kidete kutetea haki za wananchi wa Sudan Kusini. Mashtaka haya hayana msingi wa kisheria,” alisema msemaji wa chama cha SPLM-IO, ambacho Machar anakiongoza.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema hatua hii inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mustakabali wa mchakato wa amani nchini humo, huku baadhi wakionya kwamba kuondolewa kwa Machar kunaweza kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuamsha tena mapigano ya kijeshi.

Sudan Kusini, Taifa changa zaidi duniani, limeendelea kukabiliwa na misukosuko ya kisiasa na kiusalama tangu kujipatia uhuru wake mwaka 2011. 

Watazamaji wa kimataifa sasa wanafuatilia kwa karibu mwenendo wa kesi hii, wakihofia kwamba mivutano kati ya Kiir na Machar inaweza kurudisha nyuma juhudi za kuliletea taifa hilo amani ya kudumu. 




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top