Nairobi, Kenya
Serikali ya Kenya imetangaza kuwa ndege ya rais, maarufu kama Harambee One, itastaafishwa rasmi baada ya kutumika kwa zaidi ya miongo mitatu.
Habari zinabainisha kwamba ndege hiyo aina ya Fokker-70 hivi sasa iko kwenye safari yake ya mwisho ya matengenezo makubwa nchini Uholanzi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Harambee One imekumbwa na changamoto nyingi za kiufundi kwa miaka ya karibuni, ikiwa ni pamoja na matatizo ya mfumo wa majimaji (hydraulic system), milango kushindwa kufunguka ipasavyo, pamoja na gharama kubwa za matengenezo.
Aidha, upatikanaji wa vipuri vya ndege hiyo umekuwa mgumu kutokana na umri wake, jambo lililochangia uamuzi wa serikali kuiondoa kwenye huduma.
Waziri wa Ulinzi Bi.Soipan Tuya amenukuliwa akisema "Harambee One imelitumikia taifa kwa heshima na uaminifu kwa zaidi ya miaka 30. Lakini sasa tumefikia wakati ambapo gharama za kuiendesha zimekuwa kubwa kuliko thamani yake.Sheria inaturuhusu kubadilisha ndege ya Rais kila baada ya miaka miwili hivyo ni jukumu letu kuhakikisha Rais anatumia usafiri ulio salama, wa kisasa na unaoendana na hadhi ya taifa."
Ndege hiyo ilianza kutumika rasmi mwaka 1995, wakati wa utawala wa Rais mstaafu Daniel arap Moi, na imekuwa ikitumika na marais wote waliomfuatia – Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta na sasa Rais William Ruto.
Hata hivyo, serikali bado haijatangaza ndege mbadala kwa ajili ya safari rasmi za rais. Kwa sasa, imedokezwa kuwa shughuli za rais zitaendelea kwa kutumia ndege za Kenya Air Force, safari za kibiashara, au ndege binafsi kutegemea mahitaji.
Wachambuzi wa masuala ya usafiri wa anga wanasema hatua ya kustaafisha Harambee One ni ya kawaida, ikizingatiwa kuwa ndege hiyo imehudumu kwa muda mrefu zaidi ya viwango vya kawaida vya ndege za kifahari za serikali.