Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesisitiza kuwa, Chama cha ACT-Wazalendo, hakina mgombea urais wala makamu wa urais.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima imeeleza hivi:
“Katika tovuti rasmi ya Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT -Wazalendo) taarifa iliyotolewa tarehe 21 Septemba, 2025, imeonesha uwepo wa Mkutano wa Uzinduzi wa Ilani ya Uchaguzi ya ACT- Wazalendo katika Makao Makuu ya Chama hicho na kufuatiwa na Mkutano wa Uzinduzi wa Kampeni za Ubunge katika Jimbo la Segerea.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, shughuli zote mbili zitahudhuriwa na waliotajwa kama wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Luhaga Joelson Mpina na Ndugu Fatma Abdulhabib Ferej.
Tunasisitiza kwamba, chama cha ACT-Wazalendo hakina wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa kuzingatia uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wa tarehe 15 Septemba, 2025 uliotengua uteuzi wa Ndugu Luhaga Joelson Mpina aliyependekezwa na Chama hicho kugombea Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Baada ya uamuzi huo, aliyekuwa mgombea wa Kiti cha Rais na Chama cha ACT-Wazalendo walijulishwa kwa barua kuhusu uamuzi huo wa Tume.
Hivyo, taarifa ya chama cha ACT-Wazalendo inayoeleza uwepo wa wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais siyo sahihi.
Aidha, taarifa ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Segerea, ambaye ndiye mratibu wa Ratiba za Kampeni za Ubunge, inaonesha kuwa hakuna ratiba ya kampeni za mgombea ubunge wa Chama cha ACT- Wazalendo katika eneo lililotajwa katika taarifa ya ACT- Wazalendo.
Tunashauri na kusisitiza kuwa, Chama cha ACT Wazalendo kizingatie masharti ya Kanuni ya 35 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 inayohusu utaratibu na ratiba za kampeni za ubunge.”