22 Septemba 2025
Mbozi – Machifu wa kimila Wilayani Mbozi katika maeneo ambapo mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Ruanda hadi Idiwili unapita, wameupokea mradi huo kwa mikono miwili na kuahidi kuulinda, kuutunza na kushirikiana nao ili kuhakikisha unakamilika kwa mafanikio.
Akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi ya mradi huo, Mpewa Nzunda, Chifu wa Idiwili, alisema wao kama viongozi wa kimila wako tayari kuupokea mradi huo na kutoa onyo kali kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kuikwamisha miradi ya maendeleo.
“Mtu yeyote atakayethubutu kuhujumu au kukwamisha mradi huu, sisi kama viongozi wa kimila tutashughulika naye kwa taratibu zetu. Huu ni mradi wa maendeleo kwa manufaa ya vizazi vyote,” alisema Chifu Nzunda.
Kwa upande wake, Chifu Mwamlima wa Iyula aliwataka wakandarasi wa mradi huo, ambao ni wanawake, kushirikiana kwa karibu na viongozi wa kimila na wananchi katika kutatua changamoto zitakazojitokeza, ikiwemo tatizo la wizi wa vifaa vya ujenzi.
“Wizi ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo. Tunawaomba wakandarasi washirikiane nasi ili changamoto kama hizo zitatuliwe mapema na kazi iendelee kwa ufanisi,” alisema.
Akitoa shukrani kwa mapokezi mazuri waliyoyapata, Mkandarasi Bi Debora Sengati alisema wamefarijika kuona viongozi wa kimila na wananchi wakiwa mstari wa mbele kushirikiana nao.
Naye Bi Never Black Mwakalinga, mmoja wa wakandarasi, alibainisha kuwa ushirikiano na machifu ni nguzo muhimu kwa sababu wao wanafahamu vyema mazingira, changamoto na suluhisho za maeneo husika.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Ruanda–Idiwili ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na wakandarasi wanawake wazawa, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwashirikisha wanawake katika miradi ya barabara ili kuwawezesha kiuchumi.
Aidha, machifu hao walimpongeza Rais Dkt. Samia kwa kuwaletea mradi huo muhimu unaotarajiwa kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Mbozi na maeneo jirani, huku wakimshukuru pia Mbunge wa zamani wa Vwawa, Japhet Hasunga, kwa mchango wake katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo ya jimbo hilo.