Dkt Lekashingo awataka Watanzania kuchangamikia fursa katika sekta ya madini

GEORGE MARATO TV
0

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, amewataka Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana katika Sekta ya Madini ili kujiongezea kipato na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa.


Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea mabanda kwenye Maonesho ya Nane ya  Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita, Dkt. Lekashingo amesema:

“Sekta ya Madini ni injini muhimu ya uchumi wa taifa letu. Hatuwezi kuiacha mikononi mwa wageni pekee, ni lazima sisi kama Watanzania tujitokeze kwa wingi, tuchangamkie fursa zilizopo kuanzia utafiti, uchimbaji, uchenjuaji hadi kwenye biashara na utoaji wa huduma migodini. Tukifanya hivyo, tutajipatia kipato na kuisaidia nchi kuongeza Pato la Taifa.”


Ziara hiyo imehusisha pia viongozi mbalimbali wa Tume ya Madini wakiwemo Makamishna wa Tume, Mhandisi Theonestina Mwasha na Dkt. Theresia Numbi; Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki; Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Idfonce Masoud pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Mjiolojia Samwel Shoo.


Dkt. Lekashingo amebainisha kuwa uwepo wa migodi mikubwa umefungua fursa nyingi ambazo Watanzania wanapaswa kuzijenga kwa ubunifu na weledi. 

“Katika migodi hiyo kuna nafasi za usambazaji wa vifaa vya uchimbaji, vyakula, ulinzi, vifaa kinga, na hata ajira za moja kwa moja. Hii ni nafasi yetu, tusisite kuichangamkia,” amesisitiza.

Aidha, amepongeza sekta binafsi, hususan kampuni kubwa za uchimbaji wa madini, kwa kuwaamini Watanzania na kuwapa zabuni za utoaji huduma. 

Hata hivyo, amewataka watoa huduma kuwa waadilifu. “Uaminifu ndiyo mtaji mkubwa katika biashara. Nasisitiza tena: Watanzania, fanyeni kazi zenu kwa uadilifu na ubora, ili waajiri na wawekezaji waendelee kutuamini,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Lekashingo na ujumbe wake wakiwa katika banda la Wizara ya Madini na Taasisi zake wamejionea shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu sera na sheria za madini, tafiti za kijiolojia, taratibu za upatikanaji wa leseni za madini, biashara ya madini, uongezaji thamani madini, pamoja na usimamizi wa mazingira katika shughuli za uchimbaji.

Kwa mujibu wa Tume ya Madini, maonesho hayo yamekuwa chachu ya kutoa elimu na kuunganisha Watanzania na wawekezaji, lengo likiwa ni kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha wananchi wengi zaidi kupitia ajira, biashara, na mapato ya Serikali.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top