Geita – Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, ameipongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kuja na wazo la kuanzisha mradi mkubwa wa Makazi ya Biashara mkoani Geita, akisema hatua hiyo ni tafsiri ya maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora.
Akizungumza mara baada ya kutembelea maonyesho ya nane ya teknolojia ya madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita, Kingalame alisema mradi huo ni fursa muhimu ya maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla
“Makazi haya yataleta raha kwa sababu watumishi na wananchi kwa ujumla watapata makazi bora ya kuishi. Hii ndiyo tafsiri ya Rais Dkt. Samia anatamani watu wake wakae kwenye maeneo mazuri,” alisema Kingalame.
Aidha, amewapongeza TBA kwa uamuzi wa kukaribisha sekta binafsi kushirikiana nao katika utekelezaji wa mradi huo, akisema ushirikiano huo utasaidia kukamilisha makazi hayo kwa muda muafaka.
“Naitaka sekta binafsi ichangamke ije kushirikiana na TBA ili makazi haya yakamilike kwa wakati. Ni wakati wa kila mmoja kushiriki katika kuboresha maisha ya Watanzania,” alisisitiza.
Mradi huo wa Makazi ya Biashara mkoani Geita unatarajiwa kuongeza fursa za uwekezaji, kuboresha mazingira ya makazi kwa watumishi na wananchi, na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kanda ya ziwa.