Mamlaka ya Maji safi Na usafi wa mazingira Bukoba BUWASA wamekamilisha utekelezaji wa mradi wa maji ambao umegharimu Bilioni 3.1 ambao utanufaisha wananchi zaidi ya elfu 18,000 wa kata tano za manispaa ya Bukoba na moja Halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera
Mratibu wa Mradi huo Daudi Byeyanga akitoa taarifa ya kukamilika kwa mradi huo mbele ya Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2020 na kusema kuwa mradi huo mekamilika kwa asilimia Mia moja.
Amesema huo ni mradi ambao unaenda kuondoa Adha kwa wananchi wa kata za pembezoni mwa Mji wa Bukoba ambazo zilipata maji kwa mgao na kata nyingine kutoka Halmashauri ya Bukoba ikiwemo kata Kahororo,Buhembe Nshambya ,Kashai na Nyakato
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ussi amewataka wananchi kutunza miundo mbinu ya miradi ya maji na vyanzo vya maji Ili miradi hiyo iweze kudumu muda mrefu.
Amesema serikali itahakikisha Kila mwananchi anayeishi mjini anaunganisha maji Nyumbani kwa bei nafuu na mwananchi anayeishi kijijini Anatetembea mita 400 tu kufata maji.
Swaum Seveline ni mmoja wa wanawake wa kata ya Buhembe ulipojengwa mradi huo ameishukuru Serikali kuleta mradi huo maana umekuwa mkombozi kwao kwasababu walikuwa wakipata changamoto ya kufuata maji kwenye vijito vya asili ambavyo hutumiwa na wanadamu na mifugo.
"Maji ni maendeleo kwasasa hatupotezi muda mwingi kufuata maji umbali wa kilomita 16 watoto walipotumwa kufuata maji walitembea saa mbili na zaidi sasa tunatumia maji safi na salama karibu na makazi yetu, ukilinganisha na huko nyuma ambapo tulifua nguo mara moja kwa mwezi hari iliyosababisha kuliwa na
chawa kutokana na uchafu "amesema Swaum.