Na Shomari Binda-Musoma
CHAMA cha Mapinduzi ( CCM) mkoa wa Mara kimepanga kugawa kadi za kielekronicki kwa wanachama wake 645,000 kuanzia machi 29.
KATIBU wa Siasa, Uenezi,Itikadi na Mafunzo Mkoa wa Mara Simon George Rubugu amesema kuwa Chama hicho kimepokea kadi za wanachama wa mkoa huo waliosajiliwa kwa mfumo wa Kielektroniki zipatazo 645,000 ambapo kinatarajia kuanza zoezi la ugawaji wa kadi hizo.
Rubugu ameyasema hayo leo Machi 27, 2025, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake.
Amesema kadi hizo zimebooreshwa kisasa huku akitoa msisitizo kwa wanachama wa CCM ambao bado hawajasajiliwa kujisajili kwani zoezi hilo ni endelevu.
Kiongozi huyo amesema idadi ya kadi hizo ni zaidi ya asilimia 51 ya makisio ya wapiga kura na zitasaidia kuwatambua wanachama wa Chama cha Mapinduzi kuanzia ngazi ya matawi, Kata, Wilaya hadi Mkoa kabla ya kuingia katika uchaguzi unaotarajia kufanyika mwaka huu.
"Kadi hizi zitakuwa na faida kwa wanachama ikiwemo kuwatambua wanachama wote kwenye mfumo, urahisi wa kufanya nao mawasiliano, Mwanachama kuitumia kadi katika matumizi ya miamala hivyo naomba wanachama wakati wanakwenda kuchukua kadi zao waende na vitambulisho vyao vya NIDA au kadi ya mpiga kura kwa ajili ya kuingizwa kwenye mfumo.
"Tunashukuru sana juhudi thabiti zilizofanywa na Mwenyekiti wetu Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wanachama wanakuwa kwenye mfumo na haya ni mageuzi makubwa na mazuri sana kwa chama chetu ." amesema Rubugu.
Pia amepongeza miradi ya maendeleo iliyofanywa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo ujenzi wa miradi ya Kimkakati kama uwanja wa Ndege wa Musoma, Daraja la Magufuli Mwanza, Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, miradi mbalimbali ya elimu, afya, barabara, maji ambayo amesema itakipa ushindi wa kishindo chama hicho kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.
"Miradi ambayo imefanywa na serikali uhakika ni kwamba chama kitashinda kwa ushindi mkubwa sana, hii ndio reforms ya maendeleo miradi inaonekana kwa macho. mkoa wa Mara tunao uwanja wa Ndege ambao utafungua fursa ya uchumi. tunao mradi mkubwa wa maji wa Mugango-Kiabakari- Butiama huu umesaidia wananchi wengi na mradi mwingine wa maji upo wa Rorya unakwenda mpaka Tarime wa bilioni134, wananchi wamekoshwa na miradi hii."ameongeza.
Aidha amewataka wanachama wa chama hicho mkoa wa Mara kuendelea kushikamana, kupendana na kuachana na makundi madogo madogo. Ili waendelee kuyasema kwa wananchi mema na maendeleo yote ambayo serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inayafanya maeneo mbalimbali hapa nchini.







