Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo, amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga, kuhakikisha mkandarasi wa barabara ya Isongole-Isoko anaanza ujenzi mara moja.
Tayari serikali imetangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Isongole II – Ibungu – Isoko (km 52.419) kwa kiwango cha lami, ambapo waathiriwa wa mradi wapatao 312 wamelipwa jumla ya TZS milioni 850.269 kama fidia ya mali, nyumba, na mazao yao.
Barabara hiyo ni muhimu kwani itasaidia kuunganisha mikoa ya Mbeya na Songwe, hivyo kurahisisha usafiri na biashara mipakani, kati ya mpaka wa Kasumulu wilayani Kyela, Mkoa wa Mbeya, na Isongole wilayani Ileje na Tunduma wilayani Momba, Mkoa wa Songwe, ambazo zinapakana na nchi za Malawi na Zambia.