Na Ghati Msamba, Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesema Serikali mkoani hapo itaendelea kuunga mkono shughuli za maendeleo ya wanawake.
Amesema hayo wakati alipokuwa akifungua Mkutano wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara (TWCC) katika Ukumbi wa Uwekezaji, ulio Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Serikali inazo fursa nyingi kwa ajili ya wanawake, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa hapa nchini kwa ajili ya makundi maalum ya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu,” amesema Kanali Mtambi.
Kanali Mtambi ameongeza kuwa Serikali imeweka mazingira mazuri, ikiwemo sera, sheria, kanuni, na taratibu zinazowawezesha wanawake kufanya shughuli zao, hususan shughuli za uzalishaji mali, bila kubaguliwa.
Aidha, amewataka wanawake kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika Mkoa wa Mara, ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii, na uchimbaji wa madini ili kujikwamua kiuchumi.
Amewataka wanawake wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ikiwa ni pamoja na kuwania nafasi mbalimbali zinazogombaniwa na kupiga kura ili kumchagua Rais, wabunge, na madiwani.
Amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuhakikisha kuwa wanawake wa Mkoa wa Mara wanapata nafasi ya kushiriki maonesho ya Kitaifa na Kimataifa.
Akitoa risala kwa Mkuu wa Mkoa, Katibu wa TWCC Mkoa wa Mara, Anastazia Kirati, amesema wanawake wajasiriamali wanakutana na changamoto katika kupata mikopo kutoka kwa taasisi za kifedha, changamoto inayowakwamisha maendeleo ya biashara zao. Anastazia ameomba Mkuu wa Mkoa kusaidia kupatikana kwa mikopo hii.
“Wanawake wanapata changamoto ya kupata mikopo, ambapo wapo wanaopata, lakini hawana elimu ya kutosha kuhusu namna ya kuitumia vizuri mikopo hiyo,” amesema Anastazia.
Anastazia ameomba Serikali na taasisi za kifedha kutoa elimu ya biashara kwa wajasiriamali wanaopewa mikopo ili waweze kufaidika zaidi na mikopo hiyo na kuendeleza biashara zao kuwa kubwa.
Mmoja wa wajasiriamali pia ni Katibu Msaidizi wa TWCC, Selina Sospeter, ambaye ameeleza changamoto wanazokutana nazo wanapokwenda kukopa katika taasisi za kibenki, ambapo wanatakiwa kuwa na fedha katika akaunti yao kwa muda wa mwaka mmoja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda wa TWCC, Happiness Mabula, amesema kuwa TWCC ilianzishwa mwaka 2005, na sasa inakaribia miaka 20, ikitoa huduma kwa wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali hapa nchini, na ina wanachama 200.