Na Ghati Msamba,Musoma.
Waandishi wa habari kutoka mkoa wa Mara wamepata mafunzo muhimu kuhusu uwekezaji mkubwa kutoka shirika la umma la HAIPPA PLC, lengo kuu likiwa ni kuwahamasisha Watanzania kuwekeza katika masoko halisi ili kukuza uchumi, ajira, na biashara.
Mafunzo hayo yalifanyika leo katika ukumbi wa Mwembeni, mjini Musoma, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa HAIPPA PLC, Boniphace Ndengo, alieleza umuhimu wa uwekezaji kupitia masoko ya hisa. Ndengo alisema kuwa shirika lao linajizatiti kuwa akademi bora ya kukuza uwekezaji na biashara hapa nchini na barani Afrika kwa kubuni miradi, kujenga biashara, na kuwezesha miradi mikubwa.
Lengo la HAIPPA PLC ni kufikia Watanzania 600,000 ili washiriki katika uwekezaji mkubwa kupitia kampuni za umma na miradi ya ushirikiano wa umma na binafsi (PPP), na kwa kuongeza, kusaidia kuanzisha angalau kampuni 50 za umma.
Amesema kuwa teknolojia ya mawasiliano na ushirikiano na wadau mbalimbali itasaidia kufikia Watanzania zaidi ya milioni 20 kwa lengo la kutoa elimu ya uwekezaji, hasa kupitia kampuni za umma. Elimu hii inatarajiwa kuchangia katika kukuza kipato cha Mtanzania mwekezaji (GDP per capita), kutoka wastani wa shilingi milioni 3 kwa mwaka hadi milioni 30 ifikapo mwaka 2028.
Akizungumzia kuhusu hali ya uwekezaji nchini, Ndengo alisisitiza kwamba, kwa mujibu wa sheria na sera za maendeleo ya Taifa, kuna vipengele vingi vinavyozingatia uchumi shirikishi na shindani, kuimarisha uwezo wa viwanda, kukuza biashara, na kuchochea maendeleo ya watu.
Alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi za Afrika zenye makampuni machache ya uwekezaji duniani, huku akieleza kuwa mara nyingi tafsiri ya neno "mwekezaji" imetumika vibaya, jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi.
Aidha, Ndengo alisisitiza umuhimu wa kufundisha masomo ya biashara na uwekezaji kuanzia ngazi za shule za msingi na sekondari, jambo ambalo hadi sasa halijatekelezwa ipasavyo.
Alitoa wito kwa serikali kuongeza juhudi katika kuvutia wawekezaji katika sekta muhimu kama vile kilimo, teknolojia, miundombinu, nishati, na madini.
HAIPPA PLC ilianzishwa mwaka 2022, na Julai 2023 ilianza kuwekeza katika masoko ya hisa kwa bei ya shilingi 380,000 kwa kuanzia shilingi milioni 3, na kufikia mtaji wa shilingi milioni 240 ifikapo mwaka 2024/25.
Lengo la shirika hili ni kuendeleza na kukuza uwekezaji nchini na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania.
Mmoja wa waandishi wa habari, Timothy Itembe kutoka gazeti la Nipashe alieleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili wawekezaji nchini, hususan katika mkoa wa Mara, ni mifumo mibovu inayowekwa na serikali ambayo inakwamisha juhudi za kuvutia mitaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Mara, Jacob Mugini, alifungua mafunzo hayo kwa kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa HAIPPA PLC kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema kuwa yamefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya klabu yao na shirika hilo. Aliahidi kwamba klabu hiyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa HAIPPA PLC katika jitihada za kuhamasisha elimu ya uwekezaji mkubwa kwa Watanzania, ili waweze kuboresha uchumi wao.


.jpg)



.jpg)



