Na Ghati Msamba,
SERIKALI ya Tanzania imekemea vikali tabia ya baadhi ya Watanzania kwenda kufanya kazi nje ya nchi bila kufuata utaratibu wa kisheria, ikieleza kuwa hatua hiyo inachangia kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu mahali walipo na shughuli wanazozifanya.
Hali hii inahatarisha usalama wao na pia inakuwa kikwazo kwa juhudi za serikali kuhakikisha usalama wa raia wake.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, wakati akizindua rasmi utekelezaji wa makubaliano ya kuwezesha na kuratibu ajira za Watanzania nchini Saudi Arabia, hafla iliyofanyika jana, Januari 27, 2024, katika jiji kuu la Dar es Salaam.
Akizungumza katika tukio hilo, Mheshimiwa Kikwete amesema kuwa uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Saudi Arabia unatoa fursa kubwa kwa Watanzania kufanya kazi katika taifa hilo la Kiarabu, lakini ni muhimu kuwa na utaratibu ulio wazi na wa kisheria ili kuepuka matatizo yanayoweza kutokea kwa watu wanaosafiri bila kujali sheria zilizowekwa.
“Tunaamini kwamba, kwa kushirikiana na Saudi Arabia, tutahakikisha kuwa kila Mtanzania anayekwenda kufanya kazi huko atakuwa akifuatilia taratibu zote za kisheria na kufanya kazi kwa usalama na ustawi wake,” alisema Mheshimiwa Kikwete.
Aidha, Waziri Kikwete aliendelea kusema kuwa serikali haitaruhusu wala kuvumilia Watanzania kufanya kazi au kusafiri kwenda Saudi Arabia au nchi nyingine yoyote bila kupitia kwa mawakala waliotambulika na serikali ya Tanzania pamoja na ile ya Saudi Arabia. Hii ni hatua muhimu ili kuhakikisha kwamba wanapokwenda, wanapata huduma bora na wanajua haki zao na wajibu wao.
Miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa katika ushirikiano huu ni pamoja na kuwepo kwa utaratibu wa kisasa utakaowezesha Watanzania kusafiri kwenda kufanya kazi Saudi Arabia kwa njia sahihi. Aidha, utaratibu huu utaambatana na upimaji wa afya kwa waombaji wa ajira, ambapo wote watapewa fursa ya kufanya kazi katika mazingira bora na salama, wakipata mishahara yenye staha na fursa za kujikwamua kiuchumi.
Waziri Kikwete amesisitiza kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa ajira za kigeni katika kuboresha maisha ya Watanzania na kuchangia maendeleo ya taifa. Alisema kwamba, kupitia makubaliano haya, Tanzania itakuwa na mfumo bora wa kuratibu ajira za nje na hivyo kuepuka matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza kutokana na watu kufanya kazi kwenye nchi za nje bila kufuata taratibu.
Hivyo basi, serikali imejizatiti kuunda mazingira bora kwa Watanzania wanaotaka kufanya kazi nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuboresha ushirikiano na nchi kama Saudi Arabia ili kuhakikisha ajira hizi zina manufaa kwa pande zote mbili.

.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)