Rc Mtambi Awataka Wananchi Mkoa wa Mara Kuendelea Kudumisha Demokrasia

GEORGE MARATO TV
0



 Ghati Msamba- Musoma


MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kudumisha demokrasia kama walivyofanya katika zoezi la uandikishaji, na kuhakikisha wanakamilisha zoezi la upigaji kura kwa uangalifu na kwa kufuata sheria.

Akizungumza baada ya kupiga kura katika Kituo cha Ofisi ya Kata ya Mukendo, Mtambi alisisitiza umuhimu wa kuepuka vitendo vya kupiga kura mara mbili na kufanya kampeni katika vituo vya kupigia kura. Alisema wananchi wanapaswa kuhakikisha wanarudi nyumbani mara baada ya kupiga kura, na kuepuka kurudi tena kwenye vituo vya kupigia kura, kwani hilo ni kinyume cha sheria.

"Kwa sasa tayari mimi nimepiga kura, naomba wananchi wote mliojiandikisha mkaendelee na zoezi hili ili tuweze kupata viongozi wa serikali za mitaa watakaoshirikiana nasi katika kuleta maendeleo," alisema Mtambi.

Mkuu huyo wa Mkoa pia aliwapongeza wananchi wa Mara kwa kujitokeza kwa wingi na kudumisha demokrasia, akisisitiza kuwa haki ya kila mmoja ni kumchagua kiongozi atakayesimamia maendeleo yao. Aliahidi kuwa ulinzi na usalama umeimarishwa, na zoezi hilo litaendelea hadi kutolewa kwa matokeo.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na changamoto katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, ikiwemo kukosekana kwa majina ya wapiga kura kwenye kuta, jambo lililosababisha baadhi ya wananchi kushindwa kupata majina yao.

 Hii ni hali iliyoonekana katika baadhi ya vituo vya Halmashauri ya Musoma, kama vile Ofisi ya Kata ya Nyakato na Kituo cha Mwigobero B, ambapo baadhi ya wananchi kama Zubeda Ramadhan, Christina Nestory, na Zeda Said Hamis walikumbwa na changamoto hiyo.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, alipotembelea baadhi ya vituo vya kupigia kura, aliona changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi. Aliwataka wananchi kuwa na subira na kusema kuwa kila mtu aliyejiandikisha ana haki ya kupiga kura.

Amesisitiza kuwa ulinzi na usalama umeimarishwa, hivyo aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi na kwa amani kupiga kura, ili zoezi liendelee kwa ufanisi.

Zoezi la uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa linaendelea vizuri mkoani Mara, na hadi sasa vituo vya kupigia kura viko wazi na wananchi wengi wamejitokeza kupiga kura.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top