Fresha Kinasa-Mara.
KATIKA kutekeleza majukumu yake Ofisi ya Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) Mkoa wa Mara limetoa elimu juu ya utumiaji wa Huduma hizo kwa Watumishi 30 na Wanafunzi wa Chuo Cha Afisa Tabibu 250 (COTC) kilichopo Manispaa ya Musoma Mkoani humo.
Elimu hiyo imetolewa Novemba 14, 2024 Chuoni hapo na Mwenyekiti wa Baraza hilo Mkoa wa Mara Rhobinson Wangaso na wenzake ikiwa ni moja ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza hilo la kuyafikia makundi mbalimbali kuyaelimisha juu ya matumizi sahihi ya huduma hizo.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo Wangaso amewaambia kuwa, Watumiaji wa Huduma hizo wanalojukumu la kuhakikisha wanatumia huduma hizo kwa usahihi na kuzingatia wajibu wao pamoja na haki zao.
Amesema, Mtumiaji wa Huduma za Nishati ni maji ni Mtu yeyote, kampuni ama taasisi inayotumia bidhaa zinazodhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa matumizi binafsi na siyo biashara. Huku huduma hizo akisema zinajumuisha Nishati kama umeme, gesi, mafuta na huduma za maji zinazotolewa na Mamlaka za maji maeneo mbalimbali hapa nchini.
Amesema Mtumiaji wa huduma hizo anayohaki ya kupata taarifa sahihi na zinazotosheleza huduma za Nishati na Maji zinazodhibitiwa. Ili kumwezesha kufanya maamuzi endelevu, haki ya kuchagua huduma kwa kuzingatia bei na ubora na haki ya kuelimishwa kuhusu huduma zinazotolewa ili kumpa fursa ya kuchagua huduma stahiki.
Haki nyingine amesema ni haki ya kusikilizwa na kuwasilishwa kwenye vyombo vya kufanya maamuzi, haki ya usalama wa faragha kwa kuhifadhiwa siri, kupata huduma salama na kulindwa. Pia haki ya kufidiwa iwapo amepatiwa bidhaa yenye dosari au mbovu.
"Mtumiaji wa Huduma za Nishati na Maji anahaki ya Msingi kabisa ya kupata huduma kwa ajili ya ustawi wa maisha yake. Hivyo hata bei ya huduma ni vyema zikawa nafuu ili mteja amudu kwa kuzingatia bei ambazo zimekuwa zikiidhinishwa na mdhibiti wa huduma hizo. na pia kulalamikia huduma mbovu na kudai fidia kutokana na hasara iliyosababishwa na mtoa huduma. ."amesema Wangaso.
Pia, amesema Mtumiaji wa huduma hizo anaowajibu pia kutumia huduma hizo kwa njia halali, kutunza miundombinu, kulipia ankara kwa wakati na kulalamikia huduma mbovu.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho cha Afisa Tabibu Musoma Dkt. Gaston Kitila ameishukuru (EWURA CCC) Mkoa wa Mara kwa kutoa elimu hiyo chuoni hapo ambapo amesema imewapa uelewa Watumishi na Wanafunzi juu ya mambo mbalimbali kupitia ufafanuzi na maswali waliyouliza na kujibiwa kikamilifu.
Pia, amaeomba elimu hiyo itolewe kwa Wananchi wengi zaidi Mkoani hapa, kwani inamanufaa makubwa katika kuwapa uelewa sahihi ya matumizi ya huduma za Nishati na maji.



