Vijana 2,100 wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) kutoka Bara na Zanzibar wameanza matembezi ya siku 5 ya mshikamano, ya kilomita 200, ya kumbukizi ya miaka 25 ya kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ili kushiriki kilele cha kitaifa cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2024.
Vijana hao wameanza matembezi hayo leo kutoka Kijiji cha Mwitongo, alikozaliwa Mwalimu Julius Nyerere, kuelekea Jijini Mwanza, huku wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani hapa, Mary Joseph.
Rehema Sombi, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, amesisitiza vijana na jamii kwa ujumla kuendelea kudumisha amani iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere ili kuendelea kunufaika na matunda ya uhuru wa nchi yetu. Sombi ameiomba jamii kushiriki mchakato wa kujiandikisha na kushiriki uchaguzi, na vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara, Mary Joseph, ametumia nafasi hiyo kuwasisitizia vijana kuwa siasa ya CCM ni fursa ya uchumi. Hivyo, wanapaswa kuunda vikundi na kuchangamkia fedha za mikopo kwa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu, ambapo asilimia 10 ya makusanyo ya ndani ya halmashauri inatengwa kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.
Ameshukuru uongozi wa UVCCM Taifa kwa kuamini UVCCM Mkoa wa Mara, na kuwahakikishia kwamba hawatakosea, kwa vile wamejindaa kikamilifu.
Nae Katibu wa UVCCM Taifa, Joketi Mwegero, amesema lengo la vijana hao wa UVCCM kufanya matembezi haya ni kutoa hamasa kwa vijana kujitokeza kwa wingi ili waweze kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, na kuwaenzi viongozi wetu kwa kudumisha umoja, amani, na upendo.
Akiwatakia heri ya Mwenyezi Mungu na matembezi mema, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vikijini, Prof. Sospeter Muhongo, amechangia katoni 200 za maji ya kunywa kwa ajili ya safari ya matembezi. Amesema safari hii ni ya kihistoria kutokana na maandalizi alipoanzia mchakato wa kutafuta uhuru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa nchi yetu na kujikwamua kutoka mikono ya utumwa wa wakoloni, ambapo harakati hizo ziliaza matunda.
Prof. Muhongo amesema vijana walioshiriki matembezi ya mshikamano kuanzia Mwitongo, alikozaliwa Mwalimu Nyerere, kuelekea Mwanza, wametia hamasa ya mfano wa kuigwa kwa wenye nia ya kufanya hivyo na ni moyo wa hali ya juu wa kizalendo.