Shirika la Utangazaji Nchini Comoro (ORTC) limeelezea utayari wake katika kushirikiana na Shirika la Utangazaji la Tanzania(TBC) pamoja na la Zanzibar(ZBC) ili kuboresha mahusiano ya kihistoria na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ORTC, Hablani Assoumani alipomkaribisha Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Saidi Yakubu katika makao makuu ya Shirika hilo.
Bwana Hablani alimueleza Mhe. Balozi Yakubu kuwa Shirika lake lina dhamira ya kuwa na vipindi vya Kiswahili na pia kuonesha tamthilia na burudani kutoka Tanzania na ndio sababu wana makubaliano maalum na Shirika la ZBC yaliyosainiwa mwezi Julai na pia TBC ambayo yanahitaji kuhuishwa.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Yakubu alimueleza kuwa makubaliano yao na ZBC yanatoa fursa pia ya kubadilishana ujuzi na wataalamu kwa vipindi maalum na ni wakati muafaka viongozi wa juu kutembeleana kwa faida ya pande zote mbili.
Katika kikao hicho, Mhe. Balozi Yakubu alipata pia fursa ya kutembelea studio kadhaa na kujionea namna ORTC wanavyoandaa vipindi vyao.