Na Angela Sebastian
Waziri wa kilimo Hussein Bashe anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha siku ya chakula duniani Kitaifa ambayo yanatarajiwa kuanza Oktoba 10 hadi 16 mwaka huu katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Hayo yameelezwa na mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa wakati akiongea na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari ofisini kwake .
Aidha hajati Mwassa amesema wananchi wa mkoa wa Kagera wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na matumizi sahii ya vyakula wanavyozalisha na badala yake huuza nje ya mkoa hari inayosababisha uwepo wa lishe duni hivyo,wanapokula chakula wanatakiwa kula chakula chenye protini ya kutosha,wanga,mafuta,matunda na mboga za majani.
"Kazi kubwa katika maonesho ya siku ya chakula duniani ni kutoa elimu ya kutosha juu ya lishe ambapo kwa sasa mkoa wa Kagera tunayo asilimia 34 ya kiwango cha lishe hivyo elimu ndiyo itakayokamilisha maana ya siku ya chakula duniani"amesema Mwassa
Amesema kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Haki ya chakula kwa wote kwa maisha bora ya sasa na yajayo ambapo mkoa umejipanga kushirikiana na Wizara ya kilimo katika kufanikisha maudhui hayo, hivyo anatumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wa Kagera na Tanzania kwa ujumla waje kutumia fursa hiyo.
Naye katibu tawala msaidizi idara ya uchumi na biashara Isaya Tendega amesema mkoa huo unazalisha tani milioni 3.4 za chakula ambapo matumizi ya mkoa ni tani laki 7.7 huku ziada ya tani mil. 2.7 zinauzwa nje.