Akizungumza juu ya kadhia hiyo huko Mwitongo Butiama Leo oktoba 12,mtoto wa Baba wa Taifa,Madaraka Nyerere amesema wasanii kujiita majina ya viongozi pengine inaweza kuwa namna nzuri ya kuwaenzi viongozi hao, lakini kwa upande mwingine hawawatendei haki wazazi wao wanaostahili heshima hiyo kwa nafasi ya kwanza.
Madaraka alitoa mfano wa msanii maarufu wa vichekesho Steve Mengere ambaye amekuwa maarufu kwa kujiita Steve Nyerere na akasema hali hiyo imeleta sintofahamu kwa baadhi ya watu wanaoijua familia hiyo vizuri.
"Hapa kuna tatizo. Sio sahihi kwa Steve kuendelea kujiita hivyo na naomba wanahabari msaidie kuliweka jambo hilo sawa kwa kuwatangaza wasanii kwa majina yao halisi," amesema Madaraka.
Amewashukuru wanajumuiya mbalimbali kwa kuheshimu mchango wa Mwalimu Nyerere katika ujenzi wa Taifa katika nafasi mbalimbali akitolea mfano Umoja wa Wahitimu waliosoma shule ya sekondari Mirambo iliyoko mkoani Tabora ambako Mwalimu Nyerere alifundisha baada ya kumaliza masomo katika Chuo Kikuu cha Makerere kati ya Mwaka 1946 na 1948.
Wakiwasilisha salamu zao nyumbani kwa Mwalimu Mwitongo, Mwenyekiti wa Jumuiya wa wahitimu wa Shule ya Sekondari Milambo (AMSHA) Derek Murusuri na mjumbe wa Bodi ya Jumuiya hiyo Abdul-razaq Badru wamesema Jumuiya hiyo imeamua kuanzisha tuzo ijulikanayo kama Tuzo ya Mwalimu ili kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere na walimu wengine wanaofanya kazi yao kwa weledi mkubwa.
Murusuri amesema ujio wa tuzo ya AMSHA utakuwa kichocheo kwa wahitimu wengine kuandaa tuzo kama hizo ili kuwapa motisha walimu wengine na kutambua mchango wao kwenye sekta ya elimu.
Mbali na tuzo iliyokabidhiwa kwa familia ya Mwalimu Nyerere, wajumbe wa AMSHA pia walitoa zawadi mbalimbali kwa shule ya Milambo Sekondari ambazo zitasaidia kuchochea ari ya kujifunza na kupata elimu masafa na taarifa mbalimbali.
Wanajumuiya ya AMSHA wakiwa kwenye eneo la mwitongo wamepata fursa ya kutembelea makumbusho ya Baba wa Taifa na kujionea shehena ya kumbukumbu za hayati Mwalimu Nyerere na baadaye kuzuru katika kaburi la Baba wa Taifa na kuweka mashada ya maua.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Sheria na Katiba ambaye pia ni Mbunge wa Butiama Jumanne Sagini ambaye aliushukuru uongozi wa AMSHA kwa kubuni tuzo hiyo na uamuzi wake wa kuikabidhi kwa familia ya Mwalimu Nyerere.
"Ninawashukuru sana wana AMSHA kwa kubuni jambo hili na natoa wito kwa wahitimu wengine kukumbuka kurudisha japo kidogo kwenye shule walizosoma," amesema.