Fahamu Ubunifu wa Majiko ya Solar Yenye Uwezo wa Kupika Chakula cha Wanafunzi Zaidi 600 Katika Shule Moja Nchini Tanzania

GEORGE MARATO TV
0



Na Emmanuel Chibasa


👉Ni teknolojia Yenye Kuleta Suluhisho ya Kupunguza Matumizi ya Kuni na Mkaa Katika Taasisi za Elimu

👉Inawezesha kupika ugali, Maharage,Makande pamoja na wali Kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wengi na wafanyakazi kwa haraka zaidi pamoja na kupunguza gharama za matumizi.


Katika dunia ya leo, nishati ya umeme jua inachukua nafasi muhimu katika kukabiliana na changamoto za mazingira, kijamii na kiuchumi na taasisi za elimu zinapokua sehemu ya matumizi haya faida zake zinaonekana wazi.

Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni agenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali mbalimbali duniani. Umuhimu wa agenda hii unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.

Umeme jua ni chanzo cha nishati kisichokua na uchafuzi wa mazingira, kwa kutumia paneli za jua, shule zinaweza kupata umeme kwa gharama nafuu kwa ajili ya shughuli zao za kila siku, ikiwa ni pamoja na kupikia chakula, hii inasaidia kuboresha lishe ya wanafunzi na kupunguza matumizi ya nishati isiyo safi kama vile kuni na mafuta.

Pia matumizi ya umeme jua katika shule yanasaidia kujenga ufahamu wa mazingira miongoni mwa wanafunzi wanapojifunza kuhusu nishati mbadala wanakuwa na ufahamu wa kuhifadhi mazingira na kupunguza athari za mabadiriko ya tabia nchi.

Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia za Mwaka 2023, idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia imekua ikiongezeka kwa kiwango kidogo kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 6.9 mwaka 2021. Kiwango hiki ni chini ya kiwango cha wastani cha dunia cha asilimia 71 kwa Mwaka 2021, ambapo nchi ya Kenya ilikua na watumiaji asilimia 23.9 huku uganda ikiwa na asilimia 0.7 ya wananchi walikuwa wanatumia nishati safi ya kupikia mwaka 2021.

Katika kukabiliana na ongezeko la uharibifu wa mazingira na mabadiriko ya tabia nchi pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia. Mkakati huu una lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Matumizi haya yanaweza pia kupunguza matatizo ya kiafya yanayotokana na moshi wa nishati za kawaida za kupikia kama vile magonjwa ya mfumo wa kupumua hasa wanawake na watoto, wanakabiliwa na magonjwa ya mfumo wa hewa kama pumu na magonjwa mengine yanayohusiana na moshi.

Takwimu zinaonyesha kuwa matumizi ya kuni na mkaa ni chanzo kikubwa cha vifo vinavyotokana na magonjwa ya kupumua hivyo umeme wa jua sio tu unatoa suluhusho la nishati lakini pia unaleta manufaa kwa afya na mazingira.

Hata hivyo, bado kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa nishati nafuu, endelevu na za uhakika kwa ajili ya matumizi mbalimbali hususani ya kupikia hasa kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania. Hali hii inasababisha wananchi wengi na baadhi ya Taasisi kuendelea kutumia nishati isiyo safi ya kupikia, jambo linaloendelea kuchochea ongezeko la athari za kimazingira, kiafya, kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Mwongozo wa Benki ya Dunia kuhusu nishati safi ya Kupikia (World Bank Multi-Tier Framework- MTF), wa mwaka 2020, nishati safi ya kupikia hupimwa kwa ufanisi, urahisi wa kutumia, upatikanaji, usalama, unafuu na yenye kiwango kidogo cha sumu. 

 Vilevile, Mwongozo wa Shirika la Afya Duniani wa mwaka 2021 umeeleza kuwa nishati safi na teknolojia hupimwa kwa viwango vya chembechembe ndogo za vumbi zenye ukubwa usiozidi 2.5ÎĽm (PM2.5) na hewa ya kaboni monoksaidi zinazotolewa.

Katika kuhamasisha jamii matumizi ya nishati ya umeme jua katika taasisi za elimu hapa nchini chama cha nishati jadidifu Tanzania (Tarea) imekua ikiwakutanisha waatalam wa nishati ya umeme jua pamoja na wadau mbalimbali kujadili fursa na matumizi ya umeme wa jua katika taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na shule kama mkakati wa kulinda mazingira, kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kupunguza gharama pamoja na vifo vitokanavyo na magonjwa ya kupumua.

Magnificat sekondari iliyopo Sanya Juu mkoa wa Kilimanjaro ni moja ya shule za sekondari nchini Tanzania ambayo imeanza kutumia teknolojia ya nishati ya umeme wa jua (Solar) kwa ajili ya kupika chakula cha wanafunzi 640 pamoja na wafanyakazi 50 na hivyo kuondokana na uchafuzi wa mazingira pamoja na kuondokana na gharama kubwa za kununua kuni kwa mwezi.

Zoltan Muellekarpe ni mkurugenzi wa kampuni ya Atmosfair Gmbh  na Prosper Magali ni mkurugenzi wa kampuni ya Watu na Umeme nchini Tanzania, wakizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Tarea kwa njia ya mtandao kuhusu uvumbuzi wa teknolojia ya jikoni ya PV ya jua kwa ajili ya taasisi nchini Tanzania, wamesema teknolojia hiyo ni suluhisho la Kupikia kwa Umeme wa Jua na imeleta mapinduzi katika upikaji katika taasisi za Afrika, ambazo zinategemea kuni kwa kiasi kikubwa.

“ Tunatumia nguvu ya jua kuleta umeme katika upikaji wa taasisi na tunatoa dhamana ya upikaji kwa kutumia umeme wa gridi na uhifadhi kama akiba.

Amesema katika shule ya Magnificat Sekondari iliyopo Sanya juu yenye wanafunzi 640 na wafanyakazi 50, gharama za kununua kuni zilifikia zaidi ya TZS 1.5 milioni (USD 600) kwa mwezi. Gharama hizi zinachukua sehemu kubwa ya bajeti ya shule, ikikwamisha mipango ya maendeleo na kuboresha huduma za elimu.” Amesema Zoltan

Hata hivyo, mfumo wa Kupikia Umeme wa Jua umenatoa suluhisho endelevu kwa changamoto hizi. Shule iliyoanzisha mfumo wa umeme wa jua wenye uwezo wa 60kWp na betri za Lithium Phosphate za 30kWh imeweza kuhamasisha matumizi ya wapishi wa umeme wa nishati ya kuhifadhi. Hii inamaanisha kwamba shule itakuwa na uwezo wa kupika chakula kma vile ugali, maharage, uji, wali kwa gharama nafuu na kwa ufanisi, huku ikipunguza madhara kwa mazingira.

Awali katibu wa chama cha nishati jadidifu Tanzania(Tarea) Matthew Matimbwi akizungumza katika mkutano huo amesema chama cha hicho kimekua kikiandaa mikutano mbalimbali kwa kushirikiana na wadau ili kutoa elimu kwa jamii na taasisi mbalimbali juu ya matumizi ya nishati jua ili kuwajengea uwezo kufahamu faida za nishati hiyo katika kupunguza gharama pamoja na uharibifu wa mazingira hapa nchini.

Oliva ni mmoja wa wadau waliohudhuria katika mkutano huo kwa upande wake ameuliza kama teknolojia hiyo ya solar kwa ajili ya kupikia inaweza pia kutumika katika kilimo cha umwagiliaji ili kusaidia wanafunzi kuendesha mradi wa kilimo ili kupata kipato.

Akizungumzia hoja hiyo Zoltan Muellekarpe amesema ubunifu huo wa matumizi ya solar kwa ajili ya kupikia katika taasisi za elimu unaweza kutumika pia katika shughuli nyingine ikiwa ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji katika eneo husika la shule.

Kupikia nishati ya umeme jua kua faida chanya ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kwa malengo yote 17 ya maendeleo endelevu(SDGs).

Kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kama vile umeme wa jua, Tanzania ina njia nzuri ya kupunguza uharibifu wa mazingira, gharama za nishati, na matatizo ya kiafya yanayohusiana na matumizi ya mkaa. Mfumo wa kupikia umeme wa jua ni suluhisho linaloweza kuleta mabadiliko chanya katika shule na taasisi nchini.

Nishati na teknolojia zinazotumika kupikia nchini ni pamoja na kinyesi cha wanyama na mabaki ya mimea, kuni,mkaa, mafuta ya taa, mkaa mbadala, bayoethano, LPG, gesi asilia, bayogesi, umeme, majiko banifu na majiko ya nishati ya jua. Kwa mujibu wa Cooking Energy Action Plan ya Mwaka 2022, asilimia 82 ya nishati kuu inayotumika nchini inatokana na tungamotaka (biomass).

Kwa matumizi ya kupikia, inakadiriwa kuwa takribani asilimia 90 ya kaya nchini hutumia nishati ya kuni na mkaa kama nishati kuu ya kupikia ambapo matumizi ya kuni ni asilimia 63.5 na mkaa ni asilimia 26.2. Asilimia 10 zilizobaki zinajumuisha asilimia 5.1 za LPG, asilimia 3 za umeme na asilimia 2.2 za nishati nyingine

Picha Kwa Hisani ya Atmosfair, Watu na Umeme Limited pamoja na AI.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top