MBUNGE wa Jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko, ameibana Serikali kueleza mkakati wake wa kuhakikisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kenyamanyori unakamilika ili kuondoa adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Akizungumza bungeni leo Mei 12,2026 wakati akiuliza swali kwa Ofisi ya Waziri Mkuu tawala za mikoa na serikali za Mtaa (TAMISEMI) Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Esther Matiko, Aliyetaka kujua Mkakati wa serikali kukamilisha Ujenzi wa kituo Cha Afya kenyamanyori.
Amesema wananchi wa Kata ya Kenyamanyori wameonyesha uzalendo mkubwa kwa kuanza ujenzi wa kituo hicho kwa nguvu zao, huku Mfuko wa Jimbo pia ukichangia fedha za kusaidia utekelezaji wa mradi huo.
“Wananchi wa Kenyamanyori wanapata changamoto kubwa kufuata huduma za afya katika maeneo ya mbali, hivyo Serikali ina mkakati gani wa dharura kuhakikisha kituo hicho kinakamilika?” alihoji Esther Matiko.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Festo Dugange, amewapongeza wananchi wa Tarime Mjini pamoja na Mbunge wao kwa juhudi walizoonyesha katika kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya afya.
“Tunawapongeza wananchi wa Jimbo la Tarime Mjini pamoja na Mheshimiwa Esther Matiko kwa kuhamasisha ujenzi wa kituo hiki cha afya katika Kata ya Kenyamanyori ambayo ipo pembezoni na mbali na huduma za afya za jirani,” amesema Dugange.
Aidha, amesema Serikali imepokea hoja hiyo na itaendelea kuandaa fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo hicho, huku akimtaka Mkurugenzi wa Tarime Mjini kutenga sehemu ya mapato ya ndani kusaidia kukamilisha mradi huo muhimu kwa wananchi.
Swali hilo kwa Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko, imeibua matumaini mapya kwa wakazi wa Kenyamanyori wanaotarajia kupata huduma bora za afya karibu na maeneo yao mara baada ya kukamilika kwa kituo hicho.

