Chomete Aomba Bilioni 14 Hospitali Ya Mwalimu Nyerere, Atoa Msisitizo Huduma za Saratani Mara

GEORGE MARATO TV
0


MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya nchini, huku akiomba kuharakishwa kwa ukamilishaji wa Hospitali ya Mwalimu Nyerere mkoani Mara kwa kuongezewa Shilingi bilioni 14.

Akichangia Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27 leo Mei 12, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Chomete ameeleza kuridhishwa na juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na usimamizi thabiti wa Wizara ya Afya chini ya Waziri Mohamed Mchengerwa.


 Amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika sekta ya afya kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa damu salama, miundombinu ya umeme katika vituo vya afya pamoja na uboreshaji wa huduma za watoto wenye changamoto za kiafya.

“Tunampongeza sana Mhe. Rais kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya. Pia tunampongeza Waziri wetu wa Afya kwa usimamizi mzuri unaoifanya wizara hii kuchangamka,” amesema Chomete.

Hata hivyo, Mhe. chomete ameeleza kuwa bado kuna changamoto ya ukamilishaji wa Hospitali ya Mwalimu Nyerere mkoani Mara, akisisitiza kuwa mradi huo ni muhimu si tu kwa wananchi wa Mara bali pia kwa maeneo jirani ikiwemo Simiyu na hata wageni kutoka nchi jirani ya Kenya.

“Tunaomba Serikali itupatie Shilingi bilioni 14 zilizobaki ili hospitali hii ikamilike kwa wakati na ianze kutoa huduma kikamilifu kwa wananchi,” amesisitiza.

Aidha, ametoa wito wa kuanzishwa kwa maabara ya uchunguzi wa saratani mkoani Mara, akieleza kuwa wagonjwa wengi hasa wanawake wanakabiliwa na saratani ya matiti, damu na shingo ya kizazi, lakini bado wanalazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma za uchunguzi.

Katika hoja nyingine, Mhe. Chomete ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote, lakini akasisitiza umuhimu wa elimu kwa wananchi ili wauelewe vizuri mfumo huo pamoja na kuhakikisha vituo vya afya vinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha.

“Ni muhimu wananchi wakapewa elimu ya kutosha kuhusu bima ya afya, lakini pia huduma ziwepo kweli pale wanapokwenda, siyo tu kuwa na kadi bila kupata tiba,” alisema.

Mbunge huyo pia aliipongeza Serikali kwa mpango wa ujenzi wa miji mipya, akisema ni hatua muhimu itakayosaidia kuboresha maisha ya Watanzania na kuongeza fursa za kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top