Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi na maboresho ya viwanja vya ndege nchini ili kuimarisha sekta ya usafiri wa anga, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za utalii na biashara ndani na nje ya nchi.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma, Waziri Mbarawa amesema kipaumbele kikuu ni ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Serengeti, ambacho kitatekelezwa kama mradi wa kimkakati wenye lengo la kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa kimataifa huku ikilinda mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupitia miundombinu rafiki kwa mazingira (green airport).
Amesema hadi Machi 2026, hatua ya awali ya uchambuzi wa wakandarasi wa kimataifa (pre-qualification) imekamilika na kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za manunuzi ya kumpata mkandarasi pamoja na mhandisi mshauri wa ujenzi wa kiwanja hicho.
“Mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Serengeti ni wa kimkakati mkubwa unaolenga kuongeza ufanisi wa sekta ya utalii, kurahisisha usafiri wa anga na kulinda urithi wa asili wa taifa letu kupitia miundombinu endelevu na rafiki kwa mazingira,” amesema Waziri Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameeleza kuwa sambamba na mradi huo, Serikali inaendelea na ujenzi na maboresho ya viwanja vya ndege mbalimbali nchini ikiwemo Musoma, Moshi, Kagera na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), ambapo kazi mbalimbali zinaendelea ikiwemo ujenzi na ukarabati wa barabara za kuruka na kutua ndege, maegesho, uzio wa kiwanja, mifumo ya taa za kuongozea ndege (AGL), pamoja na ujenzi na maboresho ya majengo ya abiria na VIP terminal.
Amebainisha kuwa katika Kiwanja cha Musoma, utekelezaji wa miundombinu umefikia asilimia 63, huku KIA ikiendelea kuboreshwa katika maeneo ya huduma za abiria na mizigo ikiwemo mizigo ya ubaridi na mizigo mikavu, sambamba na maandalizi ya miundombinu mipya ya kisasa ya uendeshaji wa kiwanja.
Aidha, kupitia Wakala wa Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Serikali inaendelea na upimaji na urasimishaji wa ardhi kwa ajili ya upanuzi wa viwanja vya ndege nchini, ambapo viwanja sita vya Kirondatal, Mvumi, Ngara, Liwale, Manyoni na Singida vipo katika hatua za kukamilishiwa hati miliki ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema Pia, Serikali imeendelea kulipa fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya upanuzi wa viwanja vya ndege, ambapo wananchi 737 wa Kipunguni na 58 wa Musoma tayari wamelipwa fidia zao, huku hatua za mwisho za ulipaji kwa maeneo mengine zikiendelea kwa mujibu wa taratibu za Serikali.
“Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya usafiri wa anga kama nguzo muhimu ya kufungua uchumi, kukuza utalii na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika anga la kikanda na kimataifa,” amesisitiza.

