MGANGA Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora (Kitete), Dkt. Joachim Lyembe ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuwasilisha bajeti aliyoieleza kuwa ni ya kimkakati katika kuboresha huduma za afya nchini, hususan mpango wa ujenzi wa hospitali mpya ya Taifa Muhimbili.
Dkt. Lyembe amesema maboresho hayo yanaakisi dhamira ya Serikali ya Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha sekta ya afya na kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.
“Wizara ya Afya ni wizara muhimu sana katika taifa lolote. Huwezi kufanya biashara, kulima wala kusoma kama huna afya njema. Afya ndiyo msingi wa uchumi na maendeleo ya taifa,” amesema Dkt. Lyembe.
Amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora inajiandaa kuanza kutoa huduma za kusafisha figo (dialysis) kwa mara ya kwanza mkoani humo, hatua aliyoeleza kuwa itasaidia kupunguza adha kwa wananchi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
“Tunategemea ifikapo tarehe 15 ya mwezi ujao kuanza rasmi huduma za dialysis katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora. Hii ni hatua kubwa sana kwa wananchi wa Tabora,” amesema.
Mbali na huduma za kusafisha figo, amesema hospitali hiyo pia inaendelea kukamilisha huduma za kibingwa za macho pamoja na matibabu ya magonjwa ya moyo ili kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa ndani ya mkoa huo.
Dkt. Lyembe amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya una mchango mkubwa siyo tu katika kuokoa maisha ya wananchi, bali pia kukuza uchumi kwa kuwa wananchi wenye afya bora wana uwezo mkubwa wa kushiriki shughuli za uzalishaji na maendeleo ya Taifa.
