DCEA Yakamata Lita 66,048 za Kemikali Bashirifu Dar

GEORGE MARATO TV
0


-Magari ya Mafuta Yatumika Kusafirisha Kemikali kwa Vibali Feki

-Cyclohexanone Yenye Uwezo wa Kuzalisha Tani 11.4 za PCP Yakamatwa

-Watuhumiwa 84 Wakamatwa Katika Operesheni ya Kitaifa ya Dawa za Kulevya

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukamata jumla ya lita 66,048 za kemikali bashirifu zilizoingizwa nchini kinyume na taratibu za kisheria katika operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Aprili 2026.

Kemikali hizo ni lita 16,048 za Cyclohexanone na lita 50,000 za Extra Neutral Alcohol (ENA). 

Hayo yamesemwa na Kamishna Jenerali wa DCEA, Bw. Aretas Lyimo, leo Mei 13, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Mamlaka, Dar es Salaam.






Amesema katika operesheni hiyo, magari mawili yaliyotumika kusafirisha kemikali hizo yamekamatwa pamoja na watuhumiwa wawili. 

"Uchunguzi umebaini kuwa kemikali aina ya Cyclohexanone ziliingizwa nchini na kampuni ya Kinglion Investment Company LTD bila kufuata mifumo ya udhibiti ikiwemo kukosa vibali kutoka mamlaka husika.

"Kemikali za Extra Neutral Alcohol (ENA) zilikuwa zinasafirishwa kwa kutumia magari ya kubeba mafuta ya petroli aina ya Scania, yaliyoandikwa “Danger Petroleum”, kwa kutumia vibali vya kughushi, magari hayo yalikuwa yakisafirisha kemikali kutoka kampuni ya Maranile Group Company Limited iliyopo Kibaha, Mkoa wa Pwani" alisema Lyimo.

Kamishna Jenerali amesema watuhumiwa waliokamatwa ni Bakira Abel Zacharia (44), dereva wa gari namba T 794 BMB lenye tela tanki T 166 AHW lililokuwa limebeba lita 30,000 za kemikali hizo, na Vicent Stephen Rashid (26), dereva wa gari namba T 568 EQF lenye tela tanki T 640 EQN lililokuwa limebeba lita 20,000.

"Mazingira ya uingizaji na usafirishaji wa kemikali hizo yanaashiria nia ya kuzichepusha kwa matumizi haramu, hususan katika utengenezaji wa dawa za kulevya kwenye maabara bubu, Kemikali ya Cyclohexanone imewahi kuripotiwa kimataifa kutumika katika uzalishaji wa dawa ya kulevya aina ya Phencyclidine (PCP)" alisema Lyimo.


Sambamba na operesheni hiyo, DCEA ilifanya operesheni katika mikoa ya Dodoma, Mtwara, Njombe, Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza na kukamata tani 5.733 za bangi, tani 1.67 za mirungi, gramu 48.23 za heroin na gramu 113.35 za cocaine, Ekari 38.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa, magari manne na pikipiki 14 kukamatwa, huku watuhumiwa 84 wakishikiliwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top