Waziri Ulega Amwaga Sifa Kwa Nyansaho Kwa Kufanikisha Billion 1.4 Kuchangwa ndani ya Saa Moja

GEORGE MARATO TV
0


 KIASI cha zaidi ya bilioni 1.4 kimekusanywa katika harambee kubwa ya kuchangia ujenzi wa shule na zahanati katika kijiji cha Musati, wilayani Serengeti mkoani Mara, hafla iliyoongozwa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega.

Harambee hiyo iliyofanyika Jumamosi (Aprili 18, 2026) imeandaliwa na Taasisi ya Nyansaho (Nyansaho Foundation) chini ya Mwanzilishi na Mwenyekiti wake, Dkt. Rhimo Nyansaho (MB) ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Akizungumza katika hafla ya harambee hiyo, ambayo ilitanguliwa na uzinduzi wa Kanisa la Waadventista Wasabato ,Musati Central pamoja na nyumba ya mchungaji, Mwenyekiti wa Nyansaho Foundation, Dkt. Rhimo Nyansaho ambaye pia ni waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa, amesema taasisi yake imejikita kusaidia miradi ya kijamii hususan elimu na afya.


Amesema miradi hiyo imejengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Nyansaho kwa thamani ya TZS 500 milioni.

Sambamba na hayo amewashukuru viongozi Mbalimbali na Wananchi kwa michango hiyo, ambapo amesema Lengo ni kujenga shule kuanzia chekechea hadi kidato cha sita ili vijana wapate elimu bora, pamoja na huduma za afya kupitia zahanati.

Kwa upande wake waziri wa Ujenzi Mhe Abdallah ulega ambaye ni Mgeni Rasmi katika hafla hiyo yeye pamoja na marafiki zake walichangia TZS 100 milioni, huku michango kutoka kwa wafanyabiashara, taasisi za fedha, wageni waalikwa na wananchi wa kawaida ikifikisha jumla ya TZS 1.4 bilioni.




Mhe. Ulega amempongeza Dkt. Nyansaho kwa mchango wake mkubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo, akimtaja kuwa mfano wa kuigwa.

“Wana Mara hongereni sana kwa kuwa na Dkt. Nyansaho. Kazi anazofanya ni kubwa na za kupigiwa mfano. Mnaye mtu wa kujivunia,”. Amesema.

Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini jenerali Jacob Mkunda ameongoza harambee hiyo ya ujenzi wa shule na zahanati ambapo yeye na Majenerali na makamishna kutoka wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga Taifa wamechangia kiasi Cha shilling Million Mia Mbili na Mbili.

"Mchango huu ni sehemu ya dhamira ya Jeshi kushirikiana na wananchi katika shughuli za maendeleo, hususan katika maeneo yanayohitaji uboreshaji wa huduma za kijamii kama elimu na Afya". Amesema

Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara kanali Evance Mtambi ameiomba Serikali Kuboresha Miundombinu ya barabara za Mkoa wa Mara ikiwemo barabara ya kutoka Serengeti kwenda Arusha kwani kuwekeza Kwenye barabara kutaleta Mafanikio makubwa katika mkoa wa Mara.

Kadhalika,Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masanju katika hafla hiyo amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na umoja wa kitaifa kama nguzo kuu katika kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Ameongeza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kulinda amani iliyopo na kushiriki kikamilifu katika kuimarisha umoja, ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta tija kwa Taifa.

Patrick Chandi, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, ameipongeza Taasisi ya Nyansaho Foundation chini ya Mwenyekiti wake Waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Dkt. Rhimo Nyansaho kutokana na hatua yake ya kujitoa na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa nyumba ya ibada, hatua inayotajwa kuwa ni ya kuigwa katika kuunga mkono maendeleo ya jamii na kuimarisha imani ya kiroho.

kupitia harambee hiyo iliyolenga kuimarisha maendeleo ya wananchi Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete, ametoa shilingi milioni mbili kama mchango wake binafsi huku akisisitiza umuhimu wa viongozi kushiriki moja kwa moja katika kuleta maendeleo ya jamii.

Mh Ghati pia ameweza kufanikisha michango kutoka kwa waheshimiwa wabunge wengine ambao waliochangia katika kuunga mkono jitihada hizo ni, Kangi Lugola Mbunge wa Jimbo la Mwibara amechangia kiasi Cha shilingi laki tano,Jafari Chege Mbunge wa Jimbo la Rorya amechangia shilingi laki saba, 

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amechangia shilingi milioni moja, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara Agnes Marwa amechangia shilingi laki tano pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani amechangia shilingi milioni moja.

Pia,Askofu Mkuu wa kanisa la Waadventista Wasabato,Benjamini Nyalana, ameishukuru Taasisi ya Nyansaho Foundation kwa kufanya tendo Jema la kumpendeza Mungu Kwa kujitoa kwake katika kuchangia nyumba ya ibada kwani kufanya hivyo ni jambo zuri la kumpendeza Mungu

Hafla hiyo ya ufunguzi wa kanisa ambao umefanyika sambamba na harambee hiyo ya kuchangia ujenzi wa Zahanati na shule ya awali hadi Sekondari ikiwa ni miradi iliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Nyansaho kwa thamani ya TZS 500 milioni imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, dini, Mila na vyama vya siasa wakiongozwa na mgeni rasmi waziri wa ujenzi Abdallah Ulega, Jaji mkuu wa Tanzania George Masanju, Mkuu wa majeshi ya ulinzi nchini Jacob Mkunda na mwenyekiti wa Taasisi ya Nyansaho Foundation ambaye pia ni waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Mhe. Dkt Rhimo Nyansaho.

















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top