Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema mwanamke imara ni msingi wa uchumi imara, akisisitiza kuwa wanawake wanapaswa kutumia vyema fursa zilizopo kujijengea uchumi wao binafsi, familia na taifa kwa ujumla.
Amesema hayo Aprili 25, 2026 alipofungua Siku ya Kafiti na Mwanamke kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dorothy Gwajima (Mb), tukio lililohusisha utoaji wa mikopo, maonesho ya bidhaa na elimu ya ujasiriamali.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa mwanamke imara ni yule anayejifunza kutoka kwa waliofanikiwa, akibainisha kuwa wanawake katika Mkoa wa Mwanza ni asilimia 51 ya wananchi kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi, hivyo wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko wakishirikiana.
“Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Wanawake wa Mwanza mkiungana hakuna litakaloshindikana,” amesema huku akiwataka wanawake kuungana ili kufikia maendeleo ya pamoja.
Aidha, amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi kupitia majukwaa ya uwezeshaji na mifuko ya maendeleo, ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Mkoa wa Mwanza umetengewa zaidi ya shilingi bilioni 3.3 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Ameongeza kuwa zaidi ya shilingi bilioni mbili zinatarajiwa kutolewa kama mikopo kwa wanawake, akiwahimiza kuitumia kwa uaminifu na kuwekeza kwenye shughuli zenye tija badala ya matumizi yasiyo ya lazima.
Mhe. Mtanda pia ameishukuru Benki ya CRDB pamoja na Kafiti Foundation kwa mchango wao katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, akibainisha kuwa taasisi hizo zimekuwa mstari wa mbele kutoa mitaji, elimu ya ujasiriamali na fursa kwa wajasiriamali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Kafiti Foundation, Bw. Mapuli Kafiti, amesema taasisi hiyo imewezesha zaidi ya wajasiriamali 300 na kufikia wanufaika zaidi ya 4,000 kwa kutoa mitaji, elimu ya ujasiriamali na mafunzo mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation Bi. Tully Esther Mwambapa, amesema wamefanikiwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 21 nchi nzima huku akiwahimiza wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa uwekezaji wenye tija ili kuimarisha familia na jamii.























