Mapinduzi ya Kidijitali:Intanet Yafikia asilimia 94,Serikali yaongeza ngugu ya Tehama

GEORGE MARATO TV
0


WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema Tanzania inapiga hatua kubwa katika safari ya kidijitali, baada ya huduma ya intaneti ya kasi kufikia asilimia 94 ya maeneo ya makazi, huku watumiaji wakifikia asilimia 85.3 ya wananchi.

Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma leo Aprili 30, 2026, Kairuki ameeleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu ya mawasiliano, hususan kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.


“Tumeongeza uwezo wa Mkongo wa Taifa kutoka 200Gbps hadi kufikia kati ya 400Gbps na 2,000Gbps kwenye njia kuu, huku maunganisho ya mipakani yakiongezwa hadi 800Gbps ili kuboresha kasi na upatikanaji wa huduma za mtandao,” amesema Kairuki.

Katika kuimarisha zaidi sekta ya TEHAMA, Serikali imetenga shilingi bilioni 12.16 kwa ajili ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, hatua inayolenga kuharakisha mageuzi ya teknolojia na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.

Mradi huo unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa kupitia uwekezaji katika taasisi na miundombinu ya kisasa, ikiwemo ujenzi wa Taasisi ya Taifa ya Teknolojia ya Kidijitali pamoja na Kituo cha Ubunifu.

“Serikali itaanzisha vituo vitano vya kanda vitakavyosambaza fursa za teknolojia kwa wananchi kwa upana zaidi,” alisisitiza.

“Pia tutaendelea kusambaza vifaa vya TEHAMA na kuimarisha mfumo wa anwani za makazi ili kurahisisha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi.”

Katika hatua nyingine, vituo 32 vya huduma za kidijitali vitaanzishwa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali mtandaoni. 

Aidha, Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Taarifa za TEHAMA (Jamii Data Lake) unatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika rasmi.

Serikali pia inaendelea kuratibu utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024–2034, unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha ubunifu na teknolojia barani Afrika.

Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 222.59 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. Kati ya fedha hizo, asilimia 94.1 zimetengwa kwa miradi ya maendeleo, ishara ya msukumo mkubwa wa mageuzi ya kidijitali.

Mgawanyo unaonesha kuwa shilingi bilioni 98.48 ni fedha za ndani, huku shilingi bilioni 110.96 zikitoka nje ya nchi, jambo linalodhihirisha kuimarika kwa ushirikiano wa kimataifa katika kukuza sekta ya TEHAMA.

Bajeti hii ya wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaweka msingi imara wa Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali, ambapo intaneti si anasa tena bali ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top