MUSOMA
MKUU wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amewataka wahitimu wa mafunzo ya kada ya ualimu ngazi ya stashahada katika Chuo cha Musoma Utalii College kutumia maarifa na ujuzi walioupata kwa weledi mkubwa, ili kuchochea maendeleo ya elimu na kuwajenga watoto kuwa nguzo imara ya Taifa la kesho.
Akizungumza katika hafla ya mahafali ya wahitimu hao kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Chikoka amesema ualimu ni wito wa kipekee unaohusisha malezi, uongozi na ujenzi wa kizazi chenye maadili na maarifa yatakayochangia maendeleo ya Taifa.
Amesema: “Ualimu si kazi ya darasani pekee, bali ni dhamana ya kuibeba kesho ya Taifa. Ninyi mna jukumu la kuibadili jamii kupitia watoto mnaowafundisha.”
Aidha, amewapongeza wahitimu 430, hususan waliomaliza ngazi ya stashahada (Diploma), akisisitiza kuwa mafanikio yao yametokana na juhudi, nidhamu na uvumilivu waliouonesha katika kipindi chote cha masomo yao.
Akisoma Risala mbele ya Mgeni Rasmi Kwa niaba ya wahitu wote,Mhitimu Mathias David Mwalimu Mhitimu Mathias David amesema kuwa wataendelea kuwa walinzi wa taaluma ya ualimu kwa kuhakikisha nidhamu, usalama na maadili vinazingatiwa kikamilifu pamoja na kulinda na kuenzi heshima ya taaluma ya ualimu nchini.
Wamesema :"Tunaahidi na Tutahakikisha sisi walimu tunafanya kazi kwa weledi popote tutakapopangiwa majukumu yetu".
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chuo cha Musoma Utalii, Marwa Siaga, amesema chuo kimeweka mazingira rafiki ya kujifunzia kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata msaada wa kisaikolojia, kimaadili na kitaaluma wakati wote wa masomo yao, hususan kipindi cha mitihani.
Amesema: “Tumejipanga kuhakikisha kila mwanafunzi anapata mazingira bora ya kujifunzia ili aweze kufanikisha mitihani yake kwa utulivu na ufanisi mkubwa.”
Mkuu wa Chuo hicho Chamriho Mambina amesema chuo kinaendelea kukua na kutoa mafunzo katika fani zenye mahitaji makubwa sokoni, zikiwemo ualimu wa stashahada, elimu ya awali, upishi (Catering) na uongozi wa utalii.
Amesema: “Lengo letu ni kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa vitendo, wenye uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa katika sekta mbalimbali.”
Baadhi ya wahitimu, akiwemo Mwalimu Elizabeth Balele na Mwalimu Salama Mathias, wamesema mafunzo waliyopata yamewajengea uwezo wa kutumia mbinu mpya za ufundishaji zinazozingatia mtaala ulioboreshwa.
Wamesema: “Tumejifunza mbinu bora za ufundishaji zitakazotusaidia kuwafikia wanafunzi kwa ufanisi zaidi na kuboresha matokeo ya elimu mashuleni.”
Chuo cha MUSOMA Utalii kimetajwa kuwa chuo Bora nchini katika utoaji wa Mafunzo mbalimbali huku kikitoa wahitimu ambao wameweza kupata ajira katika taasisi na idara mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999, Chuo cha Musoma Utalii College kimeendelea kutoa elimu na mafunzo kwa zaidi ya wahitimu 6,000 katika fani mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira ambapo chuo hicho Cha Musoma utalii kimetajwa kuwa chuo Bora nchini katika utoaji wa Mafunzo mbalimbali huku kikitoa wahitimu ambao wameweza kupata ajira katika taasisi na idara mbalimbali nchini na nje ya nchi.








