WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameziagiza Halmashauri zote nchini kutumia mapato ya ndani kulipa walimu wanaojitolea katika shule mbalimbali badala ya jukumu hilo kubebwa na wazazi.
Ametoa agizo hilo leo Jumamosi, Machi 14, 2026 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Kibaoni, Kata ya Kibaoni, Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi, ambako yupo katika ziara ya kikazi.
Waziri Mkuu amesema kuwa Halmashauri zina mapato ya ndani yanayoweza kusaidia kugharamia malipo ya walimu wanaojitolea pale ambapo kuna upungufu wa walimu, hivyo si sahihi jukumu hilo kubebeshwa wazazi.
“Serikali hatupaswi kuwapa wazazi jukumu la kulipa walimu wanaojitolea. Halmashauri zina mapato ya ndani; zitumike kusaidia kulipa walimu hao pale panapokuwepo na mahitaji ya ziada ya walimu,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema suala la chakula kwa wanafunzi shuleni linaendelea kuwa jukumu la wazazi kwa kuwa hata mtoto anapokuwa nyumbani hupata chakula kutoka kwa wazazi au walezi wao.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote 184 nchini kuhakikisha wanatekeleza jukumu la kusimamia na kuratibu malipo ya walimu wanaojitolea kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri zao, akisisitiza kuwa suala hilo ni jukumu la Serikali.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa viongozi katika kushughulikia changamoto na kero za wananchi katika maeneo yao.
“Ifike wakati kila mmoja lazima atimize wajibu wake. Tuache mizaha na kupuuza shida za wananchi. Viongozi lazima wawe mstari wa mbele kutatua changamoto za watu,” amesema.
Kuhusu migogoro ya ardhi, Waziri Mkuu amesema katika maeneo mengi aliyotembelea kumekuwa na malalamiko ya migogoro ya ardhi, na kubainisha kuwa baadhi ya migogoro hiyo inachangiwa na watu waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia masuala ya ardhi.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo TAKUKURU, kufuatilia kwa kina chanzo cha migogoro hiyo ili kubaini wahusika na kuchukua hatua stahiki.
“Nawaagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia kwa kina kila mgogoro wa ardhi ili kubaini chanzo chake. Tunataka kujua ni nani aliyesababisha mgogoro huo na kama kulikuwa na maslahi binafsi, hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria,” amesema.





