Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameutaka mkandarasi Jassie and Company (JASCO) kuhakikisha ujenzi wa Daraja la Mkuyuni unakamilika na kukabidhiwa ifikapo Januari 15, 2026, ili kupunguza adha wanayoipata wananchi hususan katika kipindi cha mvua.
Ulega ametoa maelekezo hayo leo, Desemba 11, 2025, mkoani Mwanza wakati wa ziara maalum ya kukagua maendeleo ya mradi huo. Ziara hiyo imefanyika kufuatia agizo la Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyemtaka Waziri kufika eneo hilo kubaini sababu za kuchelewa kwa utekelezaji wa ujenzi.
Waziri Ulega amesema Serikali haitavumilia ucheleweshaji unaowaathiri wananchi na kusisitiza mkandarasi kuongeza kasi kuhakikisha daraja linakamilika kwa viwango vinavyostahili.







