Rc Mtambi Atakakia Kheri ya Krismas na Mwaka Mpya Wananchi Mkoa wa Mara

GEORGE MARATO TV
0


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Kanali Evans Alfred Mtambi, leo tarehe 24 Disemba, amewatakia heri ya Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya wananchi wa Mkoa wa Mara, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mtambi amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuwajaalia Watanzania, ikiwemo wananchi wa Mkoa wa Mara, afya njema hadi kufikia mwisho wa mwaka na kipindi cha sikukuu.

 Ameeleza kuwa kwa muda wote Mungu amekuwa karibu na Taifa kwa kulijalia amani na usalama, pamoja na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizowawezesha wananchi kujipatia kipato kwa mwaka mzima. Hivyo, amewahimiza wananchi kutumia kipindi hiki cha sikukuu kumtukuza Mungu kwa kuwafikisha salama mwisho wa mwaka.

Sambamba na hayo, Mheshimiwa Kanali Mtambi amewatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kuwahakikishia kuwa mkoa uko salama, hivyo waendelee kusherehekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya kwa amani na utulivu. Amesisitiza umuhimu wa wananchi kulinda afya zao na rasilimali walizonazo kwa kushirikiana na Serikali.

Aidha, ameeleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Mara vipo imara na vitaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi chote cha sikukuu na kuendelea, ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unaendelea kudumishwa.

Mheshimiwa Mtambi pia amebainisha kuwa Mkoa wa Mara umejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii na rasilimali mbalimbali, hivyo amewahimiza wananchi kujitokeza kutembelea na kufurahia maeneo hayo katika kipindi hiki cha sikukuu, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vyanzo mbalimbali vya maji vilivyopo mkoani humo.

Vilevile, amewataka watumiaji wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazojitokeza mara kwa mara kipindi cha mwisho wa mwaka. Amehimiza wananchi kuendelea kuwa imara na waangalifu katika shughuli zao zote.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi, wazazi na walezi kuhakikisha wanatunza akiba ya fedha au mali zitakazowasaidia kuwaandaa watoto kurudi shuleni mwanzoni mwa mwaka ujao. Amesisitiza kuwa kipindi cha sikukuu kisiwe chanzo cha kukwamisha elimu ya watoto kutokana na ukosefu wa sare za shule au vitendea kazi muhimu vya kujifunzia.

Zaidi amewataka Wanamkoa kuendelea kuijenga Mara iliyo salama na yenye maendeleo endelevu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top