Kenya Yatangaza Matokeo ya Wanafunzi wanaotumia Mtaala Mpya wa Elimu

GEORGE MARATO TV
0

MATOKEO ya wanafunzi wa Gredi ya 9, KJSEA ndiyo yaliyokuwa ya kwanza  kutolewa rasmi kupitia Mtaala wa Utendaji na Umilisi (CBE), tukio linaloonyesha jinsi mfumo wa elimu unavyoendelea kubadilika nchini.

Zamani kupitia mfumo wa 8-4-4 wanafunzi walitilia mkazo tu alama walizozipata ila mfumo huu unajikita sana katika Vipaji na uelewa mpana wa masomo anayoyapenda mwanafunzi.

Chini ya mfumo wa CBE, mwanafunzi anatathminiwa kuanzia Gredi ya Kwanza hadi afanye KJSEA.

Chini ya uliokuwa mfumo wa 8-4-4, wanafunzi walikuwa wakifanya Mitihani ya Kumaliza Elimu ya Msingi(KCPE) ambayo alama za mtahiniwa ndizo zilikuwa zikitathminiwa katika kila somo, alama ya jumla ikiwa 500.

Hata hivyo, KJSEA inachangia tu asilimia 60 ya alama ya mtahiniwa wa Gredi ya 9. Asilimia 40 zilizosalia nazo hugawanywa ambapo asilimia 20 hutoka kwa mtihani wa Gredi ya 6 KPSEA, kisha asilimia 20 nyingine huchangiwa na alivyofanya mwanafunzi katika masomo ya vitendo shuleni.

“Mfumo huu hautegemei alama katika mtihani mmoja tu bali maendeleo ya mwanafunzi kutoka madarasa ya chini,” anasema Afisa Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Mtihani (KNEC) David Njengere.

“Mwanafunzi akiingia kwenye sekondari ya Juu atakuwa akisomea masomo yanayoandamana na nguvu na kipaji chake. Kwa hivyo, alama kwenye mtihani mmoja haitumiki kuamua matokeo yao,” akaongeza wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya KJSEA jijini Nairobi.

Wanafunzi wa Gredi ya 9 hufanya masomo tisa huku kila somo likiwa na jumla ya alama nane. Kwa hivyo, mwanafunzi ambaye amepita zaidi na kuzoa alama zote huwa na jumla ya alama 72.

Mbali na alama pia wanafunzi hutathminiwa kwa vigezo vya kutimiza matarajio kabisa, kutimiza matarajio kwa wastani, kukaribia kutimiza matarajio na kukosa kutimiza matarajio.

Mfumo huu wa elimu unalenga kuhakikisha kuwa kuna usawa kwenye mazingira ya masomo ambapo pia Kipaji na uwezo wa kila mwanafunzi hupewa kipaumbele.

Wanafunzi hasa hawazingatii ushindani wa alama katika kila somo jinsi ilivyokuwa katika enzi za KCPE.

Katika KCPE, chini ya mfumo wa 8-4-4 alama za jumla zilikuwa 500 na watahiniwa walifanya mtihani kwenye masomo ya Kiswahili, Hesabu, Kingereza, Sayansi na Elimu Jamii ambayo ilikuwa inahusisha pia somo la dini.

Matokeo ya KJSEA pia yalitolewa bila furaha na shamrashamra ambazo zilikuwa zikiandamana na kutangazwa kwa matokeo ya KCPE.

Kila mara matokeo ya KCPE yalipokuwa yakitolewa, wanafunzi walikuwa wakisherehekea pamoja na walimu na wanafunzi huku umma ukimakinikia shule zinazoongoza na zile zilizofanya vibaya.

Wanafunzi Millioni 1.3 waliofaulu watajiunga Sekondari ya Juu Januari 13,2026 ambapo masomo ya lazima ambayo watalazimika kujifunza ni pamoja na Kiswahili – Lugha, fasihi, mawasiliano,Kiingereza – Lugha, fasihi, mawasiliano, Hisabati ya hali ya juu, stadi za tatizo, Sayansi (Sciences)-Biolojia, Kemia na Fizikia, ICT / Teknolojia na Ubunifu – Kompyuta, coding, ujuzi wa teknolojia pamoja na Sanaa, Michezo na Maadili.

Mbali na Masomo  hayo ya  lazima wanafunzi watalazimika pia kuchagua kusoma somo moja au mawili kulingana na vipaji vyao ambapo masomo husika ya hiari ni 

A:Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.

Sayansi ya Kompyuta / ICT ya Kina, Uhandisi / Kuchora Kiufundi, Sayansi za Kina (Biolojia, Kemia, Fizikia) Hisabati ya Kina. 

B. Biashara na Uchumi

Masomo ya Biashara / Ujasiriamali,Uchumi (Economics),Uhasibu (Accounting),Biashara / Masoko

C. Kilimo na Mazingira

Kilimo / Bustani (Agriculture / Horticulture), Masomo ya Mazingira (Environmental Studies), Ufugaji wa Mifugo / Kilimo cha Mazao (Animal Husbandry / Crop Science)

D. Sanaa, Lugha na Utamaduni

Sanaa za Kuonesha na Kutengeneza (Visual & Performing Arts), Lugha za Kigeni (Kifaransa, Kichina, Kijerumani, n.k.), Muziki / Tamthilia / Ubunifu (Music / Drama / Creative Design)

Sekondari ya Juu inaweka mkazo zaidi kwenye ujuzi wa vitendo na stadi za maisha pamoja na kuandaa Wanafunzi  kwa elimu ya chuo kikuu, soko la ajira, au ujasiriamali.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top