DIWANI wa kata ya Bweri katika halmashauri ya Manisipaa ya Musoma mkoani Mara Mh Paul Katikiro amewataka wananchi wa kata hiyo kujenga utamaduni wa kuchangia shughuli za maendeleo badala ya kutegemea serikali pekee.
Mh Katikiro ameyasema hayo Desemba 19 mwaka huu 2025 katika kikao cha kwanza cha maendeleo ya kata kilichoboreshwa na kufanyika katika ukumbi wa chuo cha ufundi (Bweri FDC).
Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mh Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa ya maendeleo hasa katika sekta ya Elimu,Afya,Barabara pamoja na huduma nyingine za kijamii na kwamba juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono na nguvu za wananchi.
"Maendeleo hayawezi kuja kwa kutegemea serikali kwa kila Kitu,lazima uanze kisha uiambie Serikali tumeanza tumefika hapa,....kuna baadhi ya shule zinachangamoto za ukosefu wa uzio,wapo walikubali kwa kuniita diwani niende tukafanye harambee ili tuiambie Serikali tunefika hapa,hata hiyo Marekani mnayoiona hakuibuka kama uyoga ilianza kama mchicha"alisema Katikiro
Katikiro ambaye ni mwenyekiti wa kikao hicho cha Maendeleo ya kata,amesisitiza kuwa serikali haiwezi kufanya kila Kitu na kutolea mfano kuwa hata katika familia zetu wapo babu walipambana kumaliza matatizo lakini walishindwa hivyo kila kizazi kina jukumu la kufanya sehemu yake katika kukabiliana na matatizo hayo.
Kwa sababu hiyo amempongeza mbunge mstaafu wa jimbo la Musoma mjini Mh Vedastus Mathayo,mbunge wa viti maalum mkoa wa Mara mh Agness Marwa,mstahiki meya wa halmashauri ya Manisipaa ya Musoma mh Alex Nyabiti na wadau wengine wa maendeleo kwa kukubali kuchangia vifaa mbalimbali vya ujenzi kwa ajili ya ukarabati wa ofisi ya mtendaji wa kata hiyo.
Diwani Katikiro ameomba ushirikiano na viongozi wenzake wakiwemo wananchi ili kuweka mipango ya pamoja ambayo itaharakisha maendeleo ya kata ya Bweri.
Awali akizungumza katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na naibu meya wa manispaa ya Musoma mh Haji Mtete,diwani wa viti maalum katika halmashauri hiyo mh Sister Yohana,amewaomba viongozi wa kata hiyo kuacha mapambano ya kisiasa bali waelekeze nguvu zao zote katika shughuli za maendeleo.
Amesema kata ya Bweri ambayo ni lango la kuingia katika Manisipaa ya Musoma inapaswa kuwa ya mfano kwa kila nyanja ukiwemo usafi na kwamba yote yatawezekana endapo viongozi wote wanashikamana na kuwa na mipango ya pamoja.
Naye mbunge wa viti maalum mkoa wa Mara mh Agnes Mathew Marwa akizungumza kwa njia ya simu baada mh Sister Yohana kukabidhi mifuko mitano ya saruji na mchanga ili kusaidia ukarabati wa ofisi ya mtendaji wa kata hiyo iliyotolewa na mbunge huyo,amesema yupo tayari kushirikiana na viongozi wote katika kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Mbunge Agness ameomba viongozi hao kulipa kipaumbele suala la Ekimu kwa kuweka mikakati ya kuwezesha Manisipaa ya Musoma na mkoa wa Mara unafanya vizuri katika mitihani ijayo.
Wakati huo huo Diwani Katikiro amesema anajipanga katika kukabiliana na matukio ya uhalifu ndani ya kata ya hiyo kwa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi.
Ametoa wito kwa wazazi kukaa na vijana wao kuwahimiza umuhimu wa amani,ulinzi na usalama na kwamba kamwe hawezi kukubali kuona wananchi wake wakiishi kwa hofu ndani ya kata hiyo.











