Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amezidi kuchanja mbuga kumnadi na kumwombea kura Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan ambapo ilikuwa zamu ya Iringa Mjini na Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa.
Akiwahutubia mamia ya wananchi katika mikutano miwili akianzia Kijiji cha Kidamali Jimbo la Kalenga na kuhitimisha Uwanja wa Mwembe Togwa, Iringa mjini, Septemba 13, 2025, Wasira amesema maendeleo makubwa yatashuhudiwa mkoani humo kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025-2030 ndani ya miaka mitano ijayo.
Kupitia mikutano hiyo Wasira alimwombea kura Dk. Samia ili aendeleze kasi ya maendeleo aliyoianza miaka minne na nusu iliyopita, pia aliwaombea kura wagombea ubunge Fabian Ngajilo (Iringa mjini) na Jackson Kiswaga (Kalenga) pamoja na madiwani waliosimamishwa na Chama.