Ofisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali imesema itahakikisha inatekekeza maelekezo ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania katika kutunga sheria ambazo zinalinda haki na utu wa mtu,umoja wa kitaifa,demokrasia na kuchochea ukuaji wa uchumi ikiwa ni sehemu ya utekekezaji wa dira ya taifa 2050.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Samwel Maneno ametoa kauli hiyo septemba 11 mwaka huu jijini dodoma katika kikao kazi ambacho kimehusisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini na ofisi hiyo.
Maneno amesema kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhakikisha Jamii inapata habari sahihi kutoka kwenye vyanzo sahihi na kwa wakati sahihi.
“Habari mnazoziandika zinahamasisha umoja na mshikamano kuendelea kuwepo nchini? Mkilitambua hilo ndo mtaweza kufahamu ni Habari gani Jamii ina kiu ya kuisikia kuhusu yale ambayo yanafanywa na serikali na yale ambayo yako kwa mujibu wa sheria sanjari na yale ambayo wananchi wanapaswa kuyafanya kama wajibu wao na yale ambayo ni haki yao pia ya kisheria”alisema Maneno.
Katika hatua nyingine,Naibu Mwanasheria Mkuu wa serikali amesema kuwa katika mwaka uliopita wa fedha ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemo kufanikiwa kuandaa miswada 19 ya kisheria pia imetafsiri sheria 433 kati ya 446 zilizopo hapa nchini kutoka kwenye lugha ya kiingereza kwenda kwenye lugha ya kishwahili.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwapa wananchi uwanda mpana wa kuzisoma sheria hizo na kuzielewa ili kutambua umuhimu wa utii wa sheria bila shuruti.
Tafsiri za sheria 13 zilizosalia inaendelea ambapo Naibu mwanasheria mkuu wa serikali amesema kuwa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali itaendelea kuwajengea wananchi uwezo zaidi wa kuzifahamu sheria hizo.
Pia amesema wamefanikisha maazimio mawili katika Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania na urekebu wa sheria 466 nchini ambapo kwa sasa zimeshazinduliwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na zinafanya kazi.
Aidha ofisi hiyo imefanikisha upekuzi wa mikataba 3,446 ya kitaifa na kimataifa ambayo inahusisha ununuzi,ujenzi,ukarabati na utoaji wa huduma za Jamii.
Naye Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano serikalini,ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali Leila Mhanji amesema kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kuwafahamisha wahariri ya vyombo vya habari majukumu yanayotekelezwa na ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali na kujenga mahusiano ya karibu baina ya ofisi hiyo na wahariri.
Naye mwakilishi wa msemaji mkuu wa serikali Rodney Tadeus,amewahimiza wahariri kutumia vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali kwa kuzingatia maadili,sheria na weledi ili kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi na kamilifu hususani kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Vilevile Rodney amewataka wanahabari nchini kuendelea kufuata sheria za nchi ili Taaluma ya habari iendelee kuwa na hadhi kwa ustawi bora wa Jamii na Taifa kwa ujumla.



















