Na Mwandishi Wetu, Muheza
MGOMBEA ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA amesema wananchi wa Tarafa ya Amani, hawachagui sura ya mtu bali wanachagua mtu anayejali matatizo yao na ameaahidi kushirikiana nao kwa ajili ya maendeleo.
Akizungumza kwenye mkutano wa kunadi ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika kata ya Zirai kwenye uwanja wa Vijana, MwanaFA alisema watu wa Tarafa hiyo hawachagui mtu mradi wamechagua mwakilishi bali wanachagua mgombea anayejali changamoto zinazowakabili katika tarafa yao na namna anavyozitekeleza.
MwanaFA ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema katika kura za maoni zilizopigwa ukizijumlisha zote ni asilimia 96 ya kura alizopata.
"Watu wa milimani hamchagui mtu kwasababu nyepesi, mnachagua mtu anayetazama changamoto zenu, lakini pia mtu aliyekuwa karibu na nyie, endeleeni kukiamini Chama Cha Mapinduzi na wagombea wake, naahidi kuendelea kutatua changamoto zenu" alisema MwanaFA.
Alisema katika kata hiyo iliyokuwa na wajumbe 300 alipata kura 293 hivyo ameona ni deni kubwa kwa tarafa hiyo na kwamba ataendelea kutatua changamoto zao kwakuwa CCM imekuja na ilani yenye matumaini makubwa kwa Watanzania.
"Endeleeni kutuamini katika kura hizi mnazotupa ni deni kwetu, na Kila changamoto mlizotupa tutazifanyia kazi," alisema.
Alisema tangu aingie katika nafasi hiyo tarafa ya Amani iliyokuwa na changamoto ya kituo cha afya tayari wamepata fedha kiasi cha shilingi milioni 645 ambapo ujenzi wake utaanza pindi mchakato wa kumtafuta mzabuni utakapokamilika.
Alisema wataendelea kutengeneza maeneo korofi katika barabara ya Amani huku lami ikiwekwa kadiri serikali itakapotoa fedha.
"CCM inadhamira ya dhati ya kuwarahisishia maendeleo wananchi na hakuna chama kingine ambacho kitaleta maendeleo, endeleeni kutuamini kwa kuchagua wagombea wetu," alisema na kuongeza,
"Wale wenye kadi za kupigia kura nawaomba Oktoba 29 mtoke mkapige kura, mchagueni Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, nichagueni Mimi na Salimu Sechambo awe diwani wenu,".
Awali mgeni rasmi katika mkutano huo, Faraja Mfumo ambaye ni Mjumbe wa halmashauri ya Mkoa, aliwataka wananchi wa Tarafa ya Amani kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kwenda kuwapigia kura wagombea wa CCM.
Alisema kamwe wasijaribu kuwachagua wapinzani kwakuwa hawana sera, dira ya maendeleo lakini pia hawana utaratibu mzuri wa kupata wagombea.
"Waulizeni wakipata fursa wataletaje maendeleo?, Vyama vya upinzani wanatumia changamoto za CCM kuwalaghai kisha mnawapa kura, achaneni nao maana hawana dira ya maendeleo kuhusu kushughulika na matatizo yenu," alisema na kuongeza,
"Endeleeni kubaki CCM na kuchagua wagombea wake, kwani CCM ndicho chama kinachoweza kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi,".
Aliwaombea kura mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan akitaka wananchi wampe kura za kishindo lakini pia wamchague MwanaFA kwakuwa ameonesha dhamira ya dhati na anaguswa na maendeleo ya Muheza.
Pia alitaka wawachague madiwani wa CCM ili waweze kushirikiana na viongozi hao kuleta maendeleo.
Mgombea udiwani wa kata hiyo Salimu Sechambo alisema katika miaka mitano ya mbunge MwanaFA kata hiyo imepata miradi mingi ikiwemo kutengeneza sehemu korofi za barabara.
Alisema eneo la Kwawina ambalo magari yalikuwa yakikwama na kushindwa kupita nyakati za mvua walikarabati kwa kuweka zege kwa kutengewa fedha kiasi cha shilingi milioni 110 ambazo zilimaliza changamoto hiyo.