Na Ada Ouko, Musoma.
JESHI la polisi mkoa wa Mara limetoa pongezi na shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Hassan baada ya kuwakabidhi magari 16 maalum kwa ajili ya kurahisisha utendaji wa kazi zao.
Akizungumza mara baada ya kupokea magari hayo Mkuu wa jeshi hilo mkoani Mara Pius Lutumo, amesema kupitia Mkuu wa Jeshi hilo nchini Inspekta jenerali wa polisi Camillius Wambura ametoa magari hayi na kutaja aina magari hayo kuwa ni Toyota GXR moja la Kamanda wa polisi mkoa, Toyota land cruiser hard top mawili kwa ajili ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa, na mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia wa mkoa.
" Magari mengine ni Toyota landcruiser pickup manne na Toyota Hilux manne kwa ajili ya wakuu wa polisi na wakuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa wilaya za Musoma, Bunda, Butiama na Serengeti, Pia tumepokea magari matano aina ya GWM kwa ajili ya doria" amesema Lutumo.
Amesema kufuatia kupatikana kwa magari hayi Jeshi la polisi mkoa wa Mara linawahakikishia wananchi kuwa ufanisi wa huduma za polisi utaimarika kwa kufanya doria, operesheni mbalimbali na kuwahi katika matukio na hivyo kuhakikisha kuwa amani na utulivu wa mkoa wa Mara vinatamaraki.
Aidha amewataka maafisa waliokabidhiwa magari hayo kuyatumia vizuri kwa mujibu wa kanuni za jeshi hilo zinazotawala matumizi ya vyombo vya moto ili kukidhi matarajio.
Sambamba na hilo Kamanda Lutumo ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Mara kuendelea kutoa ushirikiano na Jeshi hilo ili kuimarisha amani na usalama wa mkoa wa Mara.







