Dc Itunda Aziagiza Shule Kutoa Chakula Kwa Wanafunzi

GEORGE MARATO TV
0


Na Mwandishi Wetu, Mbeya

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe Solomon Itunda, ameongoza kikao cha lishe cha Halmashauri ya Jiji la Mbeya  kilichowakutanisha viongozi, watendaji na wadau wa elimu na afya kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Kikao hicho kimejikita katika kujadili changamoto na hatua za kuboresha lishe shuleni na ndani ya familia.

Akifungua kikao hicho, Mh Itunda alisisitiza umuhimu wa shule zote jijini Mbeya kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi, akibainisha kuwa upatikanaji wa mlo shuleni utasaidia kupunguza utoro, kuongeza umakini darasani na kuchochea ufaulu wa kitaaluma. 

Aidha, alitaka hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha kila mtoto anapata lishe bora inayokidhi mahitaji ya ukuaji na maendeleo ya mwili na akili.

Mh. Itunda pia aliwataka wazazi kushiriki kikamilifu katika kufuatilia maendeleo ya kielimu ya watoto wao, badala ya kuwaachia walimu jukumu lote. 

Amesema wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia, ikiwemo chakula chenye virutubisho vya kutosha, kwa kuwa elimu bora haiwezi kufanikishwa pasipo lishe bora.

Kwa upande mwingine, aliagiza watendaji wa vijiji, kata na vitongoji kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora, hususan kwa wanafunzi na watoto wenye umri mdogo.

Amesisitiza kuwa elimu ya lishe ni nyenzo muhimu ya kujenga taifa lenye afya njema na nguvu kazi thabiti kwa maendeleo ya kiuchumi.

Mh Itunda alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia kikamilifu agenda ya lishe nchini. 

Amesema uongozi wa Rais Samia umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya lishe na kuimarisha utekelezaji wa sera na mikakati ya kitaifa, hali inayotoa matumaini ya kizazi chenye afya bora na elimu imara.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justice Kijazi,  ameahidi kuwa atasimamia maagizo yaliyotolewa na Mhe.Itunda ikiwa ni pamoja na  shule zote za jiji zinaendelea kutekeleza utoaji wa huduma ya chakula shuleni.

Kijazi amesema ofisi yake itasimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango wa lishe shuleni, na kuhakikisha wazazi na walimu wanashirikiana kwa karibu katika kuwajengea wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia.

Aidha, ameongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Mbeya itashirikiana na wadau wa maendeleo na wataalamu wa afya ili kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wananchi wengi zaidi, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto za udumavu na utoro mashuleni.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top