Na Mwandishi wetu Jovina Massano.
Mgombea udiwani kata ya Mwisenge kwa tiieti ya ACT Wazalendo Alphonce Dismas Ochieng amesema atapambania uwekezaji ili kukuza kipato na kuinua uchumi wa wananchi wa kata ya Mwisenge Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Ameyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara akinadi sera zake Septemba 18,2025 uliofanyika katika viwanja vya Mtakuja B ambapo katika sera yake amewaeleza wananchi wa kata hiyo kuwa endapo atapata ridhaa ya kuwa diwani wa kata hiyo atajitahidi kuhamasisha uwekezaji utakaoongeza ajira kwa Vijana na wanawake wa Kata hiyo.
Amesema Kata hiyo ina historia kubwa katika Taifa la Tanzania kwa uwepo wa shule ya msingi aliyosoma hayati baba wa Taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere lakini huduma za kijamii hazilizishi kwa hadhi yake.
"Miundombinu ya barabara siyo rafiki kiasi ambacho kinakatisha tamaa kwa wawekezaji mfano kipande cha barabara inayoelekea Zahanati ya Mwisenge kuelekea Buhare Kuna mwekezaji kaweka hoteli kubwa na kuwezesha ajira kwa jamii hasa vijana lakini barabara ni mbovu inakatisha tamaa kwa mwekezaji".
Sanjari na barabara hiyo kuna barabara ya Misango inayopita kwenye shule aliyosoma Baba wa Taifa ni mbovu imeharibika mwakilishi wa wananchi anarudi tena na kuwaeleza wananchi wampe ridhaa tena ilihali matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya kata hairidhishi nikipata ridhaa nitajitahidi kuboresha huduma hizo".
Ameendelea kusema kuwa ukosefu wa soko unapelekea huduma za majumbani kufuatwa kwenye kata za jirani ni mojawapo ya changamoto kubwa ya kiuchumi inayowakabili wananchi wa Kata hiyo.
Mbali na changamoto hiyo amesema uwepo wa maeneo makubwa ya wazi zikiwemo fukwe zikitumiwa vizuri zitawezesha ongezeko la ajira na ukuaji wa Maendeleo na kukuza uchumi kwa wananchi.
Aidha ametolea mfano wa moja ya uwekezaji uliokuwepo katika kata hiyo kuwa;
" Kulikuwa na uwekezaji mkubwa wa hoteli ya kimataifa ya Musoma hoteli ambayo hata Baba wa aliitumia kupumzika hivi sasa imekufa haifanyi kazi nitawashauri wenye Mamlaka na kuhamasisha kuifufua ili kuongeza uchumi wa Kata na ajira kwa Jamii yetu",amesema Dismas.
Mbali na uwekezaji huo ameongelea uwepo wa maeneo yaliyo wazi makubwa yenye uwezo wa kufanya uwekezaji wa soko,stendi,uwanja kwa ajili ya michezo,kituo cha Afya na uwepo wa shule ya upili(high school) utakaosaidia upatikanaji wa huduma za kijamii karibu na chanzo cha ajali.
Aidha ameongeza kuwa Kata hiyo imesahaulika sana hasa katika uboreshaji wa huduma kwa wananchi zikiwemo huduma za afya,Elimu na miundombinu ya barabara.
Sanjari na hayo ameweza kubainisha hujuma zilizofanywa na viongozi waliopita na kushindwa kuweka hadhi ya Kata kihistoria.
Kwa Upande wake Abdalla Mahmoud Songe katibu wa ACT jimbo la Musoma mjini amesema wananchi lazima wawe macho wafuatilie miradi ya iliyopo zikiwemo fedha za Maendeleo kwa kuwa fedha hizo ni za wananchi.
"Mimi kama katibu wa ACT jimbo niliekupa ridhaa ya kugombea nafasi ya kuwakilisha wananchi katika kata hii lazima uwatumikie wananchi kwa ufuatilia fedha za maendeleo bila woga", amesema Abdalla.
Amebainisha udhaifu wa diwani ambae amerudi tena kwa wananchi kuomba ridhaa kutowajibika ipasavyo kwa wananchi kwa kutotatua changamoto zilizopo kwa madai ya kurudi kuzitatua akichaguliwa tena.
Amemalizia kwa kusema kuwa endapo ACT watapewa ridhaa watawatumikia wananchi na ikitokea kutotekelezeka kwa usimamiaji huo wapo tayari kuwajibishwa.