*Na Dawati la Habari Polisi Mwanza*
Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza,Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP) Lwelwe Mpina kwa kushirikiana na Waratibu wa Polisi Jamii wa Wilaya ya Nyamagana na Misungwi mkoani humo amewatembelea wafanyabiashara wa miamala ya kifedha katika Kata ya Mkolani, Nyegezi, Nyashishi na Usagara na kuwaelimisha juu ya mbinu za kuzuia uhalifu kwenye miamala ya kifedha maeneo yao ya kazi.
Elimu hiyo imetolewa leo Septemba 19, 2025, ambapo wafanyabiashara wamehamasishwa kushirikiana na Polisi katika kulinda mali zao, kutunza mazingira ya biashara na kuchukua tahadhari dhidi ya matukio ya kihalifu.
Akizungumza na wafanyabiashara hao kwa nyakati tofauti, ACP Mpina amewasisitiza kufunga taa za kutosha na kamera za ulinzi (CCTV) kwenye maeneo zilipo biashara zao ili kusaidia ufuatiliaji wa matukio ya uhalifu na utambuzi wa wahalifu.
“CCTV ni silaha ya kisasa. Kwa sasa huwezi kuzungumzia usalama wa biashara bila kuwa na kamera za ulinzi. Zina uwezo wa kusaidia kufuatilia tukio kabla, wakati na baada ya uhalifu,” amesema ACP Mpina.
Aidha, ACP Mpina amewasihi wafanyabiashara kujenga uhusiano mwema na majirani ili kusaidiana kutoa taarifa za matukio ya kihalifu, kutumia walinzi wa kampuni binafsi waliopewa mafunzo na kuthibitishwa kisheria.
Pia amewashauri kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na vituo vya polisi pamoja na viongozi wa Serikali ya Mtaa na kutunza kumbukumbu za wateja na wageni wanaotia mashaka kwa usalama wa biashara zao.
Kwa upande wao wafanyabiashara waliopata elimu hiyo wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuwafikia moja kwa moja na kutoa elimu hiyo huku wakiahidi kutoa ushirikiano ili kuimarisha ulinzi wa biashara zao.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kusisitiza kuwa usalama ni jukumu la kila mmoja, na kutoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kutoa taarifa mapema na kushirikiana na vyombo vingine vya usalama.